Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Wakazi wa mkoa wa Arusha milioni 1.9 wanatarajia kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura la uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa ili kuweza kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa ajili ya kujiletea maendeleo katika Nyanja zote.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega amesema kuwa wananchi hao watapiga kura watakuwa na sifa ya umri wa miaka 18 na kuendelea huku wakiwa na sifa za kuwa wakazi wa eneo husika wanakojiandikishia na kupiga kura .
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo aliyefika na kujiandikisha katika daftari la kupiga kura katika kata ya Muriet ambako ni mwenyeji wa eneo hilo amesema kuwa serikali imeweka mazingira rafiki kwa watu wote kujiandikisha bila kujali itikadi za vyama vyao wote wanapaswa kushiriki katika zoezi hilo la kujiandikisha.
Msimamizi wa Uchaguzi jiji la Arusha Msena Bina amesema kuwa vituo vimefunguliwa 154 kwa ajili ya wananchi kujiandikisha hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi .
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Jonathan Shana amesema jeshi hilo litaimarisha hali ya ulinzi na usalama na kufanya kazi bila kupendelea chama chochote kama walivyotoa maelekezo kwa Askari kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo.
