Wanafunzi waliocharazwa viboko na RC Mbeya warudishwa nyumbani, kulipa Tsh. 500,000 kila mmoja


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ameamuru wanafunzi 392 wa kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kurudi nyumbani hadi Oktoba 18, 2019.

Amesema siku watakaporejea shuleni wanatakiwa kuwa na Tsh 200,000 kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa mabweni mawili ya shule hiyo yanayodaiwa kuchomwa moto na baadhi yao.

Ametoa uamuzi huo leo baada ya kufika katika shule hiyo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, siku moja baada ya kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa shule hiyo kwa madai ya kuchoma moto mabweni ya shule hiyo.

Chalamila amesema wanafunzi ambao hatatekeleza amri yake ya kulipa fedha kupitia benki na kutofika shuleni Oktoba 18, 2019, atafuatwa nyumbani kwa pingu na hataruhusiwa kufanya mtihani wake wa mwisho.

Leo Chalamila amesema wanafunzi 14 aliowachapa viboko jana ambao pia walikutwa na simu watatakiwa kulipa Tsh. 500,000 na watakaporejea shuleni waambatane na wazazi wao, kutaka fedha zote zipelekwe benki kabla ya Oktoba 18, 2019 na kupeleka risiti za malipo shuleni.

Hapo jana RC Chalamila aliwacharaza viboko wanafunzi baada ya kufika shuleni hapo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Chunya na kupewa taarifa za wanafunzi 19, wakiwemo watano wanaoshikiliwa na polisi kwamba baada ya kukutwa na simu, saa chache baadaye mabweni mawili ya shule hiyo yaliungua moto.