Watumishi wa Umma nchini watakiwa kutumia vizuri rasilimali katika utendaji kazi


Watumishi wa Umma nchini wametakiwa kutumia vizuri rasilimali zilizopo katika kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya kiutumishi iliyopo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Magu mkoani Mwanza.

“Tujenge uzalendo kwa kutumia vizuri rasilimali wezeshi katika utendaji kazi wetu, tupende na kuthamini ili kuharakisha maendeleo ya taifa” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi hao kuwa wavumilivu katika utendaji kazi kwani Serikali inatambua changamoto zinazowakabili na inaendelea kuzifanyia kazi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dkt. Philemon Sengati amemuahidi Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa kwa maslahi ya Taifa.

“Nimefarijika mno na hii ziara na nimeyapokea maelekezo kwa moyo mkunjufu kabisa, na nikuhakikishie kwamba tutaendelea kufanya kazi kwa ubunifu” Dkt. Sengati amefafanua.

Ziara ya kikazi ya Mhe. Mwanjelwa mkoani Mwanza ni utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake ya kuhimizi uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items