Waziri Mkuu atoa agizo kwa watendaji wa ngazi zote


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji katika ngazi zote wahakikishe kuwa vijana wanawezeshwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

 Ametoa agizo hilo wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa mwaka 2019 kwenye viwanja vya Mpilipili, nje kidogo ya mji wa Lindi.

“Vijana  tushirikiane na Serikali na kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo. Hatua hii itatuwezesha kama Taifa tuvuke na tufikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” amesema.

Amesema wakati anatembelea mabanda ya maonesho, ameona ubunifu wa kijana ambaye ameunda mashine ya kumsaidia mtoto njiti apate joto na pia amemuona kijana mwingine ambaye amebuni mtambo wa kupukuchua magunia 100 ya mahindi kwa saa.

Pia alitembelea banda la kikundi cha vijana kutoka China, Korea Kusini, Argentina, Arzebhaijan na Tanzania ambao waliishi kwenye mazingira magumu na wakabadilika na wameamua kushiriki maonesho hayo ili kuwabadilisha mtazamo vijana wenzao.

“Nimefurahi kuwaona hawa vijana, ninaamini watashirikiana na wenzao wa hapa kuwabadilisha vijana wa Tanzania ili wawe na fikra endelevu.”

Akizungumzia mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, imeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhouse) katika mikoa yote na Halmashauri zote nchini.

Amesema teknolojia hiyo itawasadia wakulima kupata mazao mengi katika eneo dogo na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani na nje ya nchi. “Kwa kutumia teknolojia hii, vijana wengi watapata ajira katika sekta ya kilimo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema mkakati huo ni utekelezaji wa agizo la Chama cha Mapinduzi ambacho kinatambua kuwa sekta ya kilimo ndiyo kimbilio la wananchi walio wengi na kupitia ilani yake ya mwaka 2015 Ibara ya 6 (a) imeielekeza Serikali “kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao”.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini zitenge maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana.