Waziri Prof. Ndalichako akerwa na usimamizi mbovu wa miradi ya Elimu


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameonesha kukerwa na usimamizi mbovu wa miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara anayoisimamia, Dkt. Leonard Akwilapo kuleta wataalamu watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya hiyo.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma mara baada ya kukagua baadhi ya miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango na majengo ya shule ya Msingi ya mfano Bwega kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na wizara.

"Kwa ujumla usimamizi wa Miradi katika wilaya ya Buhigwe siyo mzuri, maafisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii," alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata ramani katika ujenzi wa majengo ya shule ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.