CAG Kichere anena baada ya kukabidhiwa ofisi na Prof. Assad


Mara baada ya kukabidhiwa Ofisi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabau za Serikali(CAG), Charles Kichere amesema kuwa hatokuwa tayari kumvumilia mtu yeyote atakayeonekana kutumia mapato ya Serikali vibaya.

Amesema hayo leo wakati wa makabidhiano ya awali ya ofisi kutoka kwa CAG aliyemaliza muda wake Profesa Mussa Assad, Jijini Dar es Salaam.

"Niwaahidi tu watanzania naenda kufanya kazi, kwenda kulinda kihenge chao, nimefanyakazi TRA ninajua ugumu wa kukusanya mapato, kuja kulinda mapato nitayalinda kwa wivu mkubwa sana, sitakuwa na simile kwa watu wanaotumia mapato ya Serikali vibaya," amesema.

"Nitawaripoti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kutoa mawazo ambayo yataweza kuimarisha mihimili yetu" amesema CAG Kichere.

Kwa upande wake Profesa Assad, amemtakia heri CAG Kichere na kumuambia milango yake ipo wazi muda na siku yoyote, atakayohitaji msaada wake.

Ikumbukwe Novemba 03, 2019 Rais Magufuli alitangaza kumteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), baada ya Prof. Mussa Assad kufikia tamati Novemba 4 mwaka huu.