CCM Tabora yajigamba ushindi Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 'Hadi sasa tumeshashinda'


Asilimia 95 ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tabora, wamepita bila kupingwa baada ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora, Solomon Kasaba, alipokuwa akizungumza ofisini kwake.

Alisema hata kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo wa viongozi wa mitaa, vitongoji na vijiji, tayari asilimia 95 ya wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa na asilimia tano ndo watafanya uchaguzi.

Alisema kati ya vijiji 715 vya mkoa huo, CCM imepita bila kupingwa kwenye vijiji 675 ikiwa ni ushindi kwa asilimia 94.7 na uchaguzi utafanyika katika vijiji 38 tu sawa na asilimia 5.3.

Alisema kakati mitaa 148 ya mkoa huo, wagombea 140 wa CCM wamepita bila kupingwa ikiwa ni ushindi wa asilimia 94.5 hivyo uchaguzi utafanyika kwenye mitaa nane tu ambayo ni sawa na asilimia 5.5.

Solomoni alisema kati ya vitongoji 3,619 vya mkoa mzima wamepita bila kupingwa kwenye vitongoji 3,397 sawa na asilimia 94 hivyo uchaguzi utafanyika katika vitongoji 228 tu sawa na asilimia 6.

 “Hadi sasa tumeshashinda kwa zaidi ya asilimia 95 na tuna uhakika hata hizo asilimia 5 zilizobakia tutazichukua zote kwa kuwa wagombea wa upinzani waliopo hawazidi 10 na hawana sera yoyote na hata kampeni hawafanyi,” alisema.

Solomon alitaja vyama vitakavyochuana na CCM kuwania nafasi hizo kwa baadhi ya maeneo kuwa ni NRA, CCK, Chadema, CUF, Democratic Party, Demokrasia Makini, NCCR-Mageuzi na ADA TADEA, huku akibainisha kuwa baadhi vilizindua kampeni tu vikaishia mitini.