Dr. Kijaji aipigia Magoti UNDP kujenga visima vya maji


Na John Walter-Kondoa-Dodoma

Naibu Waziri wa fedha na Mipango ambae pia  ni Mbunge wa jimbo la Kondoa vijijini Dr. Ashatu Kijaji, ameliomba shirika la  maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP)  kuwawezesha wakazi wa kijiji cha Pahi kilichopo Wilaya ya Kondoa  Mkoani  Dodoma  kuwajengea visima  vitatu vya maji  katika shamba la halmashauri ya Kondoa  ambalo lipo ndani ya kijiji hicho kwa ajili ya kuwasaidia  kulima kilimo  cha umwagiliaji  ili  waweze kukilisha kiwanda  kipya cha alizeti kilichojengwa  kijijini hapo.

Ombi hilo limekuja mara baada ya kijiji hicho kujengewa kiwanda cha  kisasa cha kukamua mafuta ya Alizeti pamoja na kununua Alizeti  na shirika la  maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) chenye thamani ya  zaidi ya Million 51 kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa eneo hilo  kutokutembea umbali mrefu wa  kutafuta huduma ya kukamua mafuta na kuuza alizeti.

‘’Ndugu zangu nimeulizwa hapa na Bi. Christina Msisi  ambae ni mwakilishi mkaazi wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa kuwa  tunamalighafi ya kutosha? Nimemjibu  kwa nguvu zote  hatuna kwa sasa alizeti ya kutosha ya kuweza kuchakatwa kila siku, na nimuombe  mbele yenu tunaloshamba  lenye zaidi ya Ekari 2,000 kata ya jirani lile shamba ni la halmashauri tunaomba ili mradi huu uwe kweli mradi wa kuongeza mapato ya halmashauri tuwezeshe kwenye shamba lile  tupate japo visima vitatu  tufunge miundombinu ya umwagiliaji  ili tulime  mwaka mzima alizeti na kiwanda chetu kifanye kazi mwaka mzima’’alisema Dr. Kijaji. 

Chuo cha mipango vijijini kwa kushirikiana na  shirika la maendeleo  la umoja wa mataifa  kimeamua  kujenga kiwanda hicho  ambacho kitawasaidia wananchi wa Kondoa kukamua  mafuta   lakini pia kuuza alizeti yao sehemu ya karibu  bila kutumia gharama ya kusafirisha hadi mjini au kubaki kutegemea walanguzi ambao wamekuwa wakinunua alizeti hiyo kwa bei ya hasara na hii ni kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi  ambapo lengo ni kuwatoa wananchi kwenye umasikini.

Kiwanda hicho kinauwezo wa kukamua na kuchunja mafuta tani 4 na nusu za alizeti kwa siku  na mafuta yanayotoka baada ya kuchunjwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu  kutokana na  kiwanda hicho kuwa na uwezo wa kupepeta kuondoa vumbi, mchanga, mawe  pamoja na uchafu wowowte ambao umekuwa umechanganyika na Alizeti ikilinganishwa na viwanda vingine ambavyo  havina uwezo  wa kufanya hivyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda hicho Kaimu  Mkurugenzi wa chuo cha Mipango vijijini  kilichopo Dodoma Dr.Vedastus Timoth alisema kuwa kukamilika kwa kiwanda hicho ni moja ya utekelezaji wa  adhima ya  serikali ya kuifanya   Tanzania kuwa nchi ya viwanda.


Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items