Na Paschal Malulu-KAHAMA
Zaidi ya wakazi 163,293 katika halmashauri ya mji wa Kahama wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamefanikiwa kupima virusi vya ukimwi kuanzia mwezi Julai mwaka 2018 hadi Juni 2019 na kubainika walio na maambukizi watu 3,975.
Hayo yameelezwa na mratibu wa masuala ya unasihi na upimaji wa virusi vya Ukimwi halmashauri ya mji wa Kahama Grace Nzagamba ambaye amesema katika kipindi hicho cha mwezi Julai mwaka 2018 hadi Juni 2019 wanawake waliopima virusi vya ukimwi ni 91,241 huku wanaume wakiwa 72,061.
Amesema katika idadi hiyo ya watu waliojitokeza kupima afya zao waliobainika kuwa na maambukizi ni 3,975 ikiwa wanaume ni 1,356 na wanawake ni 2,619 huku akibainisha kuwa katika watu hao wengi ni kuanzia umri wa miaka 25-49.
“Idadi hiyo ukiangalia wanawake ni wengi zaidi ya wanaume ambapo karibu nusu yao lakini licha ya hilo tu idadi hiyo ya watu zaidi ya 3,000 wengi ni umri miaka 25-49 ambayo katika watu waliopima ni sawa na asilimia 30.2 kwahiyo vijana wachukue tahadhari ya Ukimwi wasiogope kupima”alisema.
Hata hivyo Grace amesema baadhi ya watu walio kwenye mahusiano wamekuwa wakiogopa kupima afya zao kitu ambacho kitaalam ni hatari kutokana na mwenza mmoja kupima na mmoja kutokupima ambapo mmoja akibainika anaweza kumwambukiza mwenzake.
Amesema watu walio kwenye mahusiano wanapopima inawasaidia kujilinda na maambukizi ya virusi vya ukimwi huku akiongeza kuwa vijana wa rika zote waendelee kujitokeza kupima na kuacha kufanya ngono isiyo salama.
