Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kufuatilia kwa kina ripoti zinazo tolewa na ofisi ya Taifa ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ili kuandika habara nzuri zenye changamoto kwa serikali na zenye kueleza majukumu yanayotekelezwa na serikali kila baada ya ripoti kutoka
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbas amesema hayo wakati akiongea na waandishi wa Habari kutoka mikoa saba (7) ya nyanda za juu kusini wakati wa warsha ya siku tatu ya toleo maalum kwa wananchi, ukusanyaji maoni na namna ya kuandika taarifa kwenye vyombo vya habari za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyofanyika Mkoani Mbeya.
Alisema waandishi wengi wa habari wamekuwa wakiripoti yaliyobainiwa na wakaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) badala ya kuyafuatilia baada ya kuibuliwa na wakaguzi ili kujua utendaji wa Serikali katika miradi mbalimbali ambayo hupitiwa na wakaguzi.
"Niwajibu wa waandishi wa habari kufuatilia na kuzungumza jitihada na hatua zinazofanywa na serikali kwa lengo la kuifahamisha Dunia mazuri yanayofanywa na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha wananchi wananufaika na nchi yao,
"Vyombo vya Habari ni mawakala wa amani na maendeleo hivyo inatakiwa vijikite katika mambo muhimu na ya msingi kwa Taifa," alisema Dkt Abas.
Akizungumzia kuhusu Taasisi zilizofanya vibaya na kusababisha kupata hati chafu na kubainika ubadhilifu wa aina yoyote, amesema serikali inaendelea kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwatumbua wanaobainika na kuiingizia serikali Hasara.
Aidha Msemaji wa Serikali amewakumbusha waandishi wa Habari kuendelea kujiendeleza kielimu kabla ya December 2021 ambapo waandishi watatambulika kuanzia ngazi ya Diploma
Mchumi ofisi ya ukaguzi hesabu za Serikal Emmanuel Philipo alitaja baadhi ya malengo ya warsha hiyo ya 6 kuwa ni kuwapa uelewa wananchi ili waweze kuichambua kwa kina ripoti ya ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali, kuwapatia nyenzo ya itakayowawezesha kushirikiana na viongozi wakiwemo Wabunge, madiwani na mabaraza katika maeneo yao wanapojadili masuala ya maendeleo yanayowahusu.
Alisema malengo mengine kuwa ni kupata makundi ya raia watakaofanya ufuatiliaji katika utekelezaji na hatimaye tathimini ya ya shughuli za umma kwa ajili ya maendeleo na kuwapatia wananchi fursa ya kutoa maoni.
