Majadiliano ya kupiga vita biashara haramu yafanyika Zanzibar


 Na Thabit Madai-Zanzibar

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto Zanzibar wamefanya majadiliano ya kupiga vita Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto nchini.

Hayo aliyasema Mkurugenzi wa Ajira  Ali Suleiman Ameir wakati wa  Majadiliano kuhusu mipango mikakati yalifanyika huko katika Ukumbi wa Mtakwimu Mkuu Mazizini  kati ya Shirika la IOM na Watendaji wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji,Wazee,Wanawake na Watoto Zanzibar.

Majadiliano hayo ya Pamoja ni moja ya shughuli zitakazotekelezwa na IOM kwa mwaka huu wa miradi 2019/2020  ikiwa ni moja ya utekelezaji wa mpango huo chini ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa Zanzibar (Zanzibar Joint Programme) kuhusu Msaada wa Maendeleo (United Nations Assistance Development Plan II 2016 -2021).

Mpango huo wa utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017-2022 Zanzibar, utasaidia Kutoa  mapendekezo  ya tafiti iliyofanywa Zanzibar na Shirika la IOM juu ya Unyanyasaji Kiuchumi ikihusisha Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Kati mipango hiyo ni  Kukuza uelewa wa jamii juu ya dhana na aina za Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, Utambuzi wa wahanga, Vyanzo na Madhara yake, Juhudi za Serikali na wadau katika utokomezaji  wa udhalilishaji huo.

Pia Mjadala huo ulihusisha Nafasi ya viongozi katika jamii juu ya utokomezaji wa ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto pamoja na biashara haramu ya usafirishaji wa Binaadamu.

Hata hivyo washiriki wa kikao hicho walipendekeza  Kuimarishwa ushirikiano wa wadau katika jamii juu ya juhudi za kutokomeza, ulinzi  wa pamoja na kuongeza mwitikio wa huduma kwa wahanga wa Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu.

Majadiliano hayo ya siku mbili  yalihusisha jumla ya washiriki 28 kutoka katika jamii, Viongozi wa Shehia, Mtaa, Viongozi wa Dini, Walimu wa Skuli za Msingi na Sekondari na Maafisa Ustawi wa Jamii.