Kocha wa Arsenal Unai Emery afurushwa kazi


Kocha wa Arsenal Unai Emery amefutwa kazi baada ya kuongoza timu hiyo kwa kipindi cha miezi 18.

Raia huyo wa Uhispania  ambaye awali alikuwa mkufunzi wa Paris St-Germain katika ligi ya Ufaransa na kushinda mataji matatu ya Europa akiwa na Sevilla, aliteuliwa kuwa mkufunzi wa Arsenal mwezi Mei 2018, akimrithi Arsene Wenger.

Mahala pake patachukuliwa kwa muda mfupi na aliyekuwa kiungo wa kati wa Arsenal Freddie Ljungberg.

Arsenal inasema kwamba uamuzi huo ulichukuliwa baada ya matokeo ya timu hiyo kushindwa kufikia kiwango kilichohitajika.

Arsenal haijashinda katika mechi saba na ilipoteza 2-1 nyumbani dhidi ya klabu ya Ujerumani Eitracht Frankfurt katika ligi ya Europa siku ya Alhamisi.