EU yaingiwa na wasiwasi kuhusu hatua ya Iran kuongeza shughuli za nyuklia

Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi kuhusiana na tangazo la Iran kuwa inapanga kupunguza zaidi ahadi zake chini ya mkataba wa nyuklia uliofikiwa na washirika wa kimataifa.

Msemaji wa ofisi ya sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic ameiomba Iran kubatilisha shughuli zite ambazo haziendani na ahadi zake chini ya mkataba wa nyuklia wa 2015 na kujizuia dhidi ya kuchukua hatua zaidi ambazo zinaweza zikahujumu udumishwaji na utekelezwaji kamili wa mkataba huo wa nyuklia.

Mapema leo, Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema kuanzia kesho Jumatano wataongeza gesi kwenye mitambo yake 1,044 ya urutubishaji Urani katika kiwanda cha Fordow.

Rouhani amesema hatua hiyo ni majibu ya moja kwa moja kwa rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo.