Halmashauri ya Mji Masasi yabuni mradi wa ufyatuaji tofali ili kuongeza mapato


Na Hamisi Abdulrahmani-Masasi

Halmashauri ya mji Masasi Mkoani Mtwara, imebuni mradi wa ufyatuaji tofali na kuziuza kwa jamii ikiwa ni mpango mkakati wa kubuni vyanzo vya mapato vya ndani ili kujiongezea mapato ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo alipokuwa akizungumza na watendaji na madiwani wa halmashauri hiyo katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa za maendeleo ya kata kwa robo ya kwanza ya mwaka.

 Alisema lengo la Halmashauri ya kubuni mradi huo ni kuwa na vyanzo vingi vya mapato vitakavyoiyongezea halmashauri hiyo mapato ya kutoka na kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ntavyo alisema mradi huo utaongeza thamani ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kwamba fedha hizo ambazo zitatokana na mradi huo wa uzaji matofali zitasaiadia kutekeleza miradi ya halmashauri.

 Alisema kwa sasa halmashauri hiyo inafyatua matofali ya inchi sita ambayo yatauzwa kwa Sh.1600 kwa tofauli moja

 Alisema matofali hayo yatauzwa kwa mtu yeyote ambaye anahitaji tofauli kwa ajili ya ujenzi hivyo kila mmoja anawajibu wa kuifahamisha jamii juu ya uwepo wa mradi huo ili uweze kuleta tija kwa halmashauri.

"Katika kubuni vyanzo vya mapato kwa halmashauri yetu tumeona tubuni mradi wa kufyatua matofali ili uweze kutuingizia fedha kupitia mapato ya ndani hii ni fahari kwetu," alisema Ntavyo

Aidha, Ntavyo aliwataka watendaji na madiwani kuendelea kuhamasisha jamii kuweza kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Ntavyo alisema serikali imekuwa ikifanya nguvu kubwa katika kuwekeza thamani ya fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

 Alisema hivyo kila mmoja kwa nafasi yake lazima atambuwe na kuchangia katika kufanikisha miradi hiyo ya maendeleo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Sospeter Nachunga alishauri watendaji na madiwani kutathimini na kusimamia vema fedha zinazotolewa na serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.