Ifahamu historia ya mwanamziki Dj Khaled

Novemba 26, 1975 alizaliwa mwanamuziki maarufu wa Marekani ambaye amekuwa akifahamika kwa jina la DJ Khaled.

Huyu ni prodyuza, DJ, mtunzi wa nyimbo na mtu anayejihusisha sana na vyombo vya habari. Jina lake halisi ni Khaled Mohamed Khaled. Alizaliwa New Orleans huko Louisiana. Khaled alianza kufahamika kwa mara ya kwanza wakati akiwa mtangazaji wa kipindi cha redio moja mjini Miami miaka ile ya 1990.

Alikuwa mtangazaji katika kipindi cha Hip hop katika Redio 99 Jamz huko huko jimboni Florida. Umaarufu wake ulilifanya kundi la Terro Squad lenye maskani yake jijini New York katika viunga vya Bronx kumkodi kwa ajili ya matamasha mubashara ya majukwaani.

Baada ya hapo Khaled alipambana na kuanza kutoa albamu ambapo mwaka 2006 aliachia albamu ya Listennn.....the Album ambayo ilijipatia cheti chenye hadhi ya juu. Mwaka uliofuata alitoa alabamu ya We the Best ambayo ilikuwa na singo 20 miongoni mwa hizo ni ile ya I’m so Hood.

Mwaka 2008 na 2010 aliachia albamu mbili ya We Global na Victory. Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuwa na lebo yake amabyo aliita We the Best Music Group. Albamu hizo mbili zilipanda vizuri katika orodha ya 10 bora za US Billboard 200; ndani hizo albamu kulikuwa na singo nyingine kali ya All I do is Win ambayo nayo ilijipatia cheti cha hadhi ya Platinum.

Mnamo mwaka 2011 aliachia albamu yake ya tano  aliyoipa jina la We the Best Forever ambayo ilifanya vizuri sokoni na kumpa umaarufu mkubwa. Kuna wimbo wa I’m on One ulifanya vizuri mno na kuwa katika orodha ya 10 bora.

Albamu ya sita na ya saba alizotoa mwaka 2012 na 2013 ambazo ni Kiss the Ring na Suffering from Success. Albamu hizo zilipanda hadi kuwa katika 10 bora za Billboard 200. Albamu ya nane aliitoa mwaka 2015 yenye jina la I changed a Lot.

Mwaka 2015 na 2016 umaarufu wa DJ Khaled ulipanda na kuushawishi ulimwengu kuanza kumfuatilia kwa kina ikiwamo mitandao ya kijamii na vituo mbalimbali vya redio na televisheni.

Aliachia albamu ya tisa mwaka 2016 ya Major Key. Albamu ya kumi aliiachia mwaka 2017 aliyoipa jina la Grateful. Mwaka huu ameachia albamu ya Father of Asahd ambayo imeshika namba mbili katika Billboard 200. Pia DJ Khaled ameandika kitabu chenye jina la The Keys ambacho kimefanya vizuri katika soko. Na mwaka ujao ataonekana katika filamu ya Bad Boys for Life.