Iraq yatangaza marufuku ya kutoka nje


Mamlaka ya mji wa Najaf nchini Iraq imetangaza marufuku ya kutoka nje baada ya kundi la waandamanaji kuuvamia ubalozi mdogo wa Iran na kuwasha moto jana jioni.

Kulingana na vyanzo vya polisi na maafisa wa ulinzi wa raia, wafanyakazi wa ubalozi huo mdogo wa Iran waliwahi kukimbia kabla ya uvamizi. Hata hivyo, shirika la habari la AP limemnukuu afisa wa polisi akisema mtu mmoja ameuawa na wengine wapatao 35 wamejeruhiwa wakati polisi walipofyatua risasi za moto dhidi ya kundi hilo la waandamanaji.

Waandamanaji hao walifanikiwa kuingia katika uwanja wa ubalozi huo wa Iran. Waliishusha bendera ya Iran na badala yake kuipandisha ya Iraq.

Iraq imekuwa na maandamano ya kuipinga serikali kwa karibu miezi miwili na zaidi ya watu 300 wamekufa kutokana na machafuko hayo.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items