Na Paschal Malulu-KAHAMA
Serikali ya halmashauri ya mji wa Kahama wilayani Kahama mkoani Shinyanga imezitaka kampuni za utengenezaji wa miundombinu ya barabara zilizoingia mkataba na halmashauri hiyo kuhakikisha zinaanza kufanya kazi iliyokusudiwa.
Akizungumzia hatua hiyo mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kahama Abel Shija amesema kampuni zaidi ya tatu ambazo zimechukua tenda ya kutengeneza barabara kupitia wakala wa barabara TARURA ndani ya halmashauri ya mji hazijaanza kazi ambapo kampuni moja ndio imeanza kazi.
Amesema kupitia wakala wa barabara vijijini na mijini TARURA kampuni hizo zimeingia mkataba wa miezi sita ambao barabara zinatakiwa kukamilika mwakani mwezi machi lakini kisiwe kigezo cha kampuni hizo kutokuanza kazi.
Shija amesema uboreshaji wa barabara ambazo zimeharibika baadhi ya maeneo yake zitafanyiwa ukarabati huo ambao utagharimu zaidi ya shilingi milioni 840 ambapo ukarabati umegusa karibu kila Kata.
Amesema lengo la mkataba wa miezi sita sio kuchelewa kuanza kazi ambapo kinachotakiwa ni kufanyika kazi kwa ufasaha na kumalizika katika muda uliopangwa kwani mkataba baina ya TARURA na kampuni hizo unaonesha zianze kazi Novemba mosi mwaka huu lakini hadi sasa bado na hakuna jitihada zinazoonekana.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha akizungumza katika baraza la madiwani halmshauri ya Msalala lililopita aliitaka TARURA kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika ili kutambua sehemu korofi kwani kutumia michoro muda mwingine inakuwa tofauti.
