Halmashauri ya Mji Masasi yakiri kupokea Tsh. Milioni 15 kuhimarisha miundombinu sekta ya elimu


Na Hamisi Abdulrahmani-Masasi

Halmashauri ya Mji Masasi Mkoani Mtwara imekiri kupokea fedha Sh. Milioni 15 zitakazotumika kwa ajili ya kuhimarisha miundombinu ya sekta ya elimu ikiwamo matundu ya vyoo vya wanafunzi na walimu katika shule zilizopo Halmashauri hiyo.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo alipokuwa akizungumza na watendaji wa kata, wakuu idara na madiwani wa Halmashauri hiyo.

Alisema wamepokea fedha hizo toka ofisi ya mkuu wa mkoa huo wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ikiwa ni gawio la kampeni yake ya shule ni choo ambayo ni fedha zinazotokana na michango ya wadau.

Alisema Halmashauri ya Mji Masasi ina changamoto kubwa ya uhaba wa matundu ya vyoo katika shule zake za msingi na sekondari hivyo fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto hiyo.

Ntavyo alisema miongoni mwa kata ambazo vijiji vyake ni kinara wa changamoto hiyo ya uhaba wa matundu ya vyoo shuleni ni Tukaewote pamoja na Temeke.

"Tunashukuru ofisi ya mkuu wa Mkoa kwa kutupatia gawio la fedha Sh. Milioni 15 kwa uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya elimu hasa matundu ya vyoo tutazitumia kama ilivyokusudiwa," alisema Ntavyo

Naye diwani wa kata ya Temeke ( CCM) Selemani Uledi aliomba Halmashauri hiyo kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu katika kata yake.

 Alisema ndani ya kata yake ya Temeke kwa baadhi ya shule za msingi miundombinu yake haijawa rafiki kwa wanafunzi na walimu hivyo jitihada za kuboresha bado zinahitajika.

Hamisi Nikwanywa diwani kata ya Mumbaka alisema sekta ya elimu ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hivyo uboreshaji wa miundombinu utasaidia kuinua kiwango bora cha elimu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, ambaye pia ni diwani wa kata ya Napupa, Sospeter Nachunga alisema Halmashauri itaendelea kupanga vipaumbele vyake katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

 Alisema fedha hizo sh.15 milioni ambazo Halmashauri imezipokea itahakikisha zinatekeleza uboreshwaji huo wa matundu ya vyoo mashuleni.

"Licha kupata fedha hizi lakini sisi kama viongozi tuendelee kuhamasisha jamii yetu kuchangia nguvu kazi zetu katika kuunga mkono haya maendeleo ili kwa pamoja tufaidike," alisema Nachunga

 Awali akizungumza na madiwani hao, katibu tawala wilaya ya Masasi, Mohamedi Azizi alisema anaipongeza Halmashauri hiyo kwa kazi mzuri za maendeleo inayozifanya.

 Alisema Halmashauri hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri kati ya watendaji na madiwani jambo ambapo limekuwa nguzo bora katika kufanikisha malengo ya kufikia maendeleo tarajiwa.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items