Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk Dorothy Gwajima, ameziagiza kamati za ujenzi na idara ya ununuzi kwenye miradi ya afya nchini, kushirikiana na wakuu wa idara za afya kununua vifaa vinavyohitajika kwaajili ya majengo yanayojengwa ili kuepuka gharama za ziada zinazojitokeza kutokana na ununuzi wa vifaa visivyotakiwa.
Dk Gwajima ametoa agizo hilo leo Novemba 4, 2019 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Rorya mkoani Mara, mradi ambao serikali imetoa jumla ya Sh1.5 bilioni kwaajili ya ujenzi wake
Amesema kuwa wamegundua kuwepo kwa ununuzi wa vifaa ambavyo haviendani na mahitaji ya kitaalam ya idara husika katika maneno mengi nchini kutokana na wataalam wa idara hizo kutokushirikishwa wakati wa manunuzi ya vifaa hivyo.
Amesema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha serikali kuingia gharama za ziada hasa wakati majengo hayo yakifikia hatua za mwisho za umaliziaji (Finishing) jambo ambalo lingeweza kuepukwa endapo wataalam hao wangeshirikishwa.
“Naziagiza halmashauri zote kuhakikisha kuwa wanawashirikisha wataalam husika wakati wa ununuzi wa vifaa vya finishing ili kuepuka gharama zisizokuwa za msingi lengo ni kuokoa fedha na muda pia,” amesema Dk Gwajima.
Amesema kuwa wamegundua kuwa maeneo mengi maafisa manunuzi wamekuwa wakinunua vifaa bila kuwashirikisha wataalam husika hivyo kujikuta wananunua vifaa ambavyo haviendani na mahitaji husika ya jengo husika.
