Madiwani wasusia kikao, Kisa halmashauri kuhamishiwa kijiji walichokikataa



Na Hamisi Abdulrahmani, Masasi

Madiwani Watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara wakiongozwa na Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, wamesusia kikao cha baraza na kutoka nje ya ukumbi kwa madai kuwa hawakubaliani na maamuzi ya serikali kuhamishia ofisi za halmashauri katika kata ya Mbuyuni.
Madiwani hao wamedai kuwa mwenyekiti na mkurugenzi wameshindwa kutoa ufafunuzi sahihi na wakimaandishi kuwa ninani ambaye ametoa idhini ya ofisi za Halmashauri hiyo kuhamia kwenye kijiji cha hicho.

Walisema maazimio ya madiwani kuhusu makao makuu ya ofisi za Halmashauri yaliamuliwa na madiwani wenyewe kuwa ofisi hizo zihamie katika mji mdogo wa Ndanda ambapo huduma nyingi za kijamii zipo ikiwemo umeme na ufasiri tofauti na Mbuyuni ambapo ofisi zimehamia kwa sasa.

Akizunguma mara baada ya kutoka nje ya ukumbi makamu mwenyekiti  Halmashauri hiyo, Nestory Chilumba ambaye pia ni diwani kata ya Mwena, alisema ameamua kutoka nje kuungana na wenzake wa nne kutokana na kutoheshimiwa mawazo yao.

"Sisi tunachojua ni kwamba baraza la madiwani likishafanya maamuzi yake na kupitisha hakuna kiongozi yoyete kuanzia ngazi ya wilaya na Mkoa ambaye anaweza kuwa na mamlaka ya kutengua isipokuwa ni waziri wa Tamisemi pekee," alisema Chilumba 

Chilumba aliongeza kuwa cha kushangaza baada ya madiwani tarehe 17 Oktoba kukaa na kufanya maamuzi ya kuhamia Ndanda hakuna kikao chochote kingine ambacho kilikaa na kufanya maamuzi mbadala ya kuhamia katika kijiji cha Mbuyuni hivyo ni nani ambaye amefanya maamuzi mengine chini ya kapeti na kuamuru ofisi hizo zihamie Mbuyuni.

Naye diwani wa kata ya Namajani ambaye pia alitoja nje ya kikao, Mashaka Salumu alisema wao wamehoji na kumtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Changwa Mkwazu kueleza kwa kutoa vielelezo vya kimaandishi vinavyoeleza ofisi za Halmashauri hiyo kuhamia Mbuyuni na sio Ndanda kama awali Madiwani walivyokaazimia Oktoba 17 kwa kupiga kura.

Salumu alisema kumekuwa na mazoea ndani ya Halmashauri hiyo viongozi ngazi ya Mkoa kuingilia maamuzi yanayofanywa na madiwani kitendo ambacho sio heshima kwa madiwani kwa sababu madiwani ndiye wenye Halmashauri sio kiongozi yeyote yule.

 Alisema sasa kama madiwani ndiye wenye mamlaka kama kanuni zinazovyosema kwa nini mawazo ya madiwani hayaheshimiwi hivyo wanapohoji kuhoji kuhusu hili na kutopewa majibu sahihi wameona bora kutoka nje ya kikao hicho ili kushinikiza kuheshimiwa michango yao.

Naye Jackson Kusanda diwani kata ya Mlingula alisema Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Gelasius Byakanwa amekuwa akiingilia maamuzi ya baraza la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Masasi.

Alisema awali mwaka jana baraza la madiwani lilifanya maazimio ya moja ya kituo cha afya kujengwa katika kijiji cha Mbuyuni lakani baadae maazimio hayo yalitenguliwa kinyemela na viongozi ngazi ya mkoa na kuelekeza kituo hicho cha afya kujengwa Chiungutwa.

 Kusanda alisema hii leo jambo lilile linajirudia kuwa madiwani walifanya maamuzi ya makao makuu ya ofisi za Halmashauri kuhamia Ndanda lakini serikali ya Mkoa imetengua maazimio yao kutaka makao makuu ya halmashauri kuhamia Mbuyuni.

 Stella Uchinga diwani viti maalumu naye alitoka nje ya kikao hicho alisema uhuru wa madiwani katika kuheshimiwa mawazo yao katika Halmashauri hiyo haupo hivyo wameamua kutoka nje ya kikao baada ya kutopatiwa majibu sahihi.

 Akitoa ufafanuzi kwa ufupi Mkurugenzi wa Halmashauri, Changwa Mkwazu alisema yeye sio ndio aliyeamuru Halmashauri kuhamia katika kijiji cha Mbuyuni bali ni agizo la serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Juma Satma alisema Madiwani hao ni lazima wafikishwe katika kamati ya maadili ili wajadiliwe kwa kitendo chao cha utovu wa nidhamu ndani ya kikao cha baraza la Madiwani na kuamua kutoka nje ya ukumbi.

Madiwani ambao wametoka nje ya kikao ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nestory Chilumba kata ya Mwena,Mashaka Salumu kata ya Namajani, Jackson Kasanda kata ya Mlingula, Hamza Kitambi kata ya Nanganga na Stella Uchinga diwani viti maalumu.