Ili uweze kuwa mfugaji bora wa kuku basi unatakiwa kuzingatia mambo ya msingi ambayo nimeyaeleza katika makala haya kama ifutavyo;
Mfumo wa banda Hili ni jambo muhimu sana unalohitajika kuwa makini nalo, haijalishi ni idadi gani ya kuku unayofuga, banda linaweza kukutengenezea au kukuharibia mafanikio katika ufugaji.
Ukifanikiwa kufanyia kazi mfumo wako wa banda utakuwa umepunguza zaidi ya asilimia 40% ya matatizo. Nimekutana na wafugaji ambao wana mabanda yasiyoridhisha. Kuku wao wamekuwa wakipata shida.
Hakikisha kuwa wewe unafanya kazi yako ya ufugaji kuwa rahisi. Kumbuka kuwa banda ndicho kitu cha pili chenye gharama nyingi ukiachana na chakula katika ufugaji.
Ulishaji na chakula Unahitaji kuzungukia kujifunza ufugaji kuku kabla hujaamua kuanza chochote, hii itakusaidia kufanikisha malengo yako, chakula na ulishaji vinachukua sehemu kubwa ya gharama za ufugaji hivyo maandalizi mazuri yatakufanya ufurahie safari yako. Unaweza kuchagua labda uzalishe chakula chako mwenyewe au ununue chakula ambacho tayari kimeandaliwa. Chakula bora kinawafanya kuku wako wakue vizuri na kuwahimarisha kinga yao ya mwili.
Kutengeneza mwenyewe chakula kunaweza kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 50%. Wafugaji wapya wasitengeneze chakula wenyewe hadi wahakikishe wamejua vizuri. Kumbuka kutengeneza chakula mwenyewe kutakugharimu kununua mashine za kufanya kazi hizo. Wafugaji wenye kuku kuanzia angalau 500 wanaweza kutengeneza chakula wenyewe kwa sababu hiyo inaweza kukulipa.
Utunzaji kumbukumbu Hili ni eneo lingine muhimu sana. Utunzaji kumbukumbu mzuri unaweza kukusaidia kukua haraka,inakusaidia kuona ulipofanikiwa na kushindwa, wapi urekebishe, weka kumbukumbu ili uweze kuongeza uzalishaji.
Baadhi ya wafugaji hawajui idadi ya kuku walionao, wangapi wamekufa..
Mabadiliko na tofauti Unahitaji kugundua tofauti katika kuku wako, hii ikihusisha ukuaji, ulishaji, kupunguza utagaji, idadi, na sauti zao.
Hii itakusaidia wewe kama mfugaji kujua mabadiliko yao. Kwa mfano: Kuku wa mayai wanapoanza kutaga hupiga kelele, ulishaji na uzito huongezeka, na muda mwingine ikiwa kuna mlipuko wa ugonjwa utagundua haraka kwa kupunguza utagaji wao, kama siyo kawaida kama siku zote basi kuna tatizo, unaweza muita mtaalamu aliye karibu nawe. Gundua mapema mabadiliko ya kuku wako.
Aina ya kuku Hili nalo ni jambo la muhimu unalopaswa kuzingatia wakati unafikiria ufugaji kibiashara. Ni kuku wa mayai au nyama? Unahitaji kuchagua kuku bora, ukizingatia na kizazi cha kuku hao.
Wapi unatilia mkazo Tunapozungumzia ufugaji kibiashara ni muhimu uwe na eneo ulilowekea mkazo. Je unataka kufuga kwajili ya kuzalisha mayai au ni nyama, au kuangulisha vifaranga, ni kwajili ya chakula kwa kuchinja na kupaki?
Mtaji Mtaji ni moja wapo ya vitu muhimu vitakavyoamua nini kifanyike. Mtaji ni kiasi cha fedha ulizowekeza katika biashara, sababu kuu kwa nini kuku wanahitaji pesa ni kuwa wanahitaji huduma nzuri ili wakuzalishie vizuri.
Vifaa vya kuku Ni vizuri kuandaa vifaa vyote kabla ya kuanza mradi ili usije kukwama. Vifaa vinavyohitajika ni: Vyombo vya chakula Vyombo vya maji Trei za mayai Chanzo cha joto(vyungu tunavyo tuwasiliane) Sehemu ya kuweka taka Chakula Dawa Eneo la kuhifadhi kuku wagonjwa.
Eneo la kufugia kuku Inatakiwa eneo ambalo lipo mbali na makazi ya watu ili kuepusha bughudha ya harufu, kuhifadhi uchafu iwe rahisi, unaweza kufuga kuku hata nyumbani kwako lakini unapofikiria kufanya mradi mkubwa wa maelfu ya kuku, jaribu kuweka mbali na makazi ya watu.
Ikiwa mambo haya yatazingatiwa, wafugaji wa Tanzania na Afrika wataona mafanikio ya wanachofanya. Hatuhitaji tena kuudharau ufugaji, bali tuuchukulie kwa umakini kama kazi nyingine