Matumizi ya mtandao yaongezeka duniani

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Mawasiliano, ITU imeeleza kuwa idadi ya watu wanaotumia mtandao wa intaneti imeongezeka kwa karibu mara nne zaidi na kufikia bilioni 4.1 tangu mwaka 2005.

Shirika hilo limeonya kuwa idadi ya wanawake wanaotumia intaneti imeshuka kwenye maeneo kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ITU iliyotolewa leo, matumizi ya mtandao wa intaneti yameongezeka ulimwenguni kwa asilimia 54.

Hata hivyo, bado watu bilioni 3.6 hawatumii mtandao huo, hasa kwenye nchi zinazoendelea.

Ripoti hiyo imeonya kuwa pengo kati ya wanaume na wanawake wanaotumia mtandao limeongezeka barani Afrika, kwenye nchi za Kiarabu na eneo la Asia na Pasifiki.

ITU imetaka hatua zichukuliwe katika kuongeza umiliki wa simu za mkononi miongoni mwa wanawake na kuanzisha ujuzi wa msingi wa kidijitali kwenye nchi zinazoendelea duniani.