Naibu Waziri wa Madini atoa siku 7 kwa walioficha Madini kuyasalimisha



Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo  ametoa siku 7 kwa walioficha madini ambayo hayana vibali  kuyasalimisha na kuyapeleka katika soko la madini ili yaweze kulipiwa kodi badala ya kusubiria operesheni kali itakayofanywa na serikali ambapo watakaokutwa na madini kinyume cha sheria madini hayo yatataifishwa pamoja na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza katika soko la madini Mkoani Arusha  baada ya kutembelea soko hilo na kujionea mwamko mkubwa wa wafanyabiashara waliofika sokoni hapo ,Naibu huyo amesema kuwa baada ya siku hizo saba hakutakua na nafasi kwani watakaokutwa wameficha madini kwa kisingizio cha kukosa soko watachukuliwa hatua kali kwani wanaiokosesha serikali mapato.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amesema kuwa serikali imeweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara waweze kupata leseni ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha kujiandikisha kupata kitambulisho cha taifa pamoja na dirisha dogo la TRA na Ofisi madini ili wafanyabiashara wote waweze kuwa na leseni.

Kwa upande wao wafanyabiashara Hussein Iddi na Karume Oweri wameitaka serikali iwalete wafanyabiashara watakaonunua madini yote bila kuchagua ikiwemo madini yenye thamani ndogo ambayo hayauziki sokoni ili kuondokana na mzigo wa madini hayo ambayo hulazimika kuyapeleka nyumbani.