Rais wa China, Xi Jinping aliyefuatana na Waziri Mkuu wa Jamaica; Ugiriki na Serbia ametembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya Pili ya kimataifa ya Bidhaa za Nje kati ya mabanda matano yaliyochanguliwa.
Katika Ziara yake katika banda hilo la Tanzania, Rais Xi Jinping alipokelewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki ambaye alitoa maelezo juu ya bidhaa mbalimbali za kilimo na madini zinazopatikana nchini Tanzania na vivutio vya utalii.
Katika ufunguzi rasmi wa maonesho hayo yalitoshirikisha mataifa 64 na kuhudhuriwa pia na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Rais Jinping aliahidi kwamba nchi yake itaendelea kufungua milango zaidi kwa bidhaa za nje kuingia katika soko la China.
Mbali na kutembelea banda la Tanzania katika maonesho hayo, Rais wa China pia alitembelea mabanda ya nchi nchi ya Ufaransa; Ugiriki; Serbia na Jamaica.
Aidha, Balozi Kairuki aliwasilisha salaam za Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa Rais wa China.
Kwa upande wake Rais wa China ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje na ametuma salaam za pongezi kwa Rais Magufuli kwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China.
Aidha, Rais Xi alivutiwa zaidi na bidhaa ya korosho za Tanzania na madini ya Tanzanite ambapo alitaka kufahamu zaidi juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko la China.Maonesho ya Kimataifa yataendelea hadi Novemba 10. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.


