Na Muhadhi mohammed, Ruvuma.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme,amesema kuwa serikali itamchukulia hatua kali za kisheria mwananchi yeyote atakayebainika kuharibu miundombinu ya barabara ikiwa pamoja na kung'oa alama za barabarani.
Mndeme aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akifungua kikao cha Bodi ya barabara cha mkoa wa Ruvuma(ROADBOARD)kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Songea mkoani humo.
Alisema kuwa kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakihujumu miundombinu ya barabara kwa kupitisha mifugo.magari yenye uzito mkubwa pamoja na kuchoma moto pembezoni mwa barabara.
Aidha ametaka kandarasi zote za ujenzi wa barabara zitolewe kwa makandarasi wenye sifa badala ya kutoa kwa makandarasi wasiokuwa na sifa ambao uchelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli kuunganisha wilaya zote kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha Lami.
Hata hivyo mkuu huyo ameigiza Tanroads mkoani humo kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayejenga daraja la mto Ruhuu wilayani Nyasa kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa wilaya za Ludewa na Nyasa.
Akichangia hoja katika kikao hicho,mstahiki meya wa manispaa ya Songea Alhaj Abdul Mshaweji ameshauri kila Halmashauri mkoani humo kuandika andiko la kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara toka vyanzo mbalimbali badala ya kuitegemea serikali.