https://monetag.com/?ref_id=TTIb ROWODO yatambulisha mradi kwa viongozi na watendaji wa wilaya ya Lindi | Muungwana BLOG

ROWODO yatambulisha mradi kwa viongozi na watendaji wa wilaya ya Lindi



Na Ahmad Mmow, Lindi.

Shirika la maendeleo ya wanawake wa Rondo( ROWODO) limetambulisha rasmi  kwa viongozi na watendaji wa ngazi ya wilaya ya Lindi, mradi wa kuwajengea uwezo wa wananchi katika ufuatiliaji wa matumizi ya raslimali za umma kwenye sekta ya maji katika kata tatu zilizopo wilayani Lindi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya utambulisho wa mradi huo, iliyofanyika leo katika manispaa ya Lindi. Mkurugenzi wa shirika hilo lisilo la kiserikali, Scholastica Nguli alizitaja kata za Namangale, Pangatena na Nyangangamara ndizo zitatekeleza mradi huo.

Alisema rasilimali za umma ni nyingi. Hata hivyo wao wamechagua kufuatilia matumizi ya rasilimali fedha katika sekta ya maji kwenye miradi inayotekelezwa katika kata hizo.

Alisema wameamua kufuatilia matumizi ya raslimali katika sekta ya maji ili kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na serikali ya kufikisha huduma ya maji safi na salama vijijini kupitia mpango wa kuwatua ndoo kichwani wanawake.


Alisema mradi huo ambao utawajengea uwezo wananchi  ili waweze kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maji na usimamizi wa vifaa vya maji kwenye kata hizo, utatekelezwa kwa kupindi cha miezi saba.

Nguli aliyataja malengo ya mradi huo kuwa ni kuhimiza uwazi na uwajibikaji wa viongozi wa ngazi za kata na vijiji, kuhusu michakato ya maendeleo na kuhamasisha jamii ishiriki uibuaji, utekelezaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo kwenye kata na vijiji vyao.

Alisema kuboreka kwa miundombinu ya maji kwenye kata hizo kutasababisha kuongezeka kwa ufanisi wa utoaji huduma kutokana na kuimarika kwa viwango vya uelewa wa jamii katika kutimiza wajibu wake katika miradi hiyo inayotekelezwa katika maeneo yake.

" Lakini pia kutakuwa na ukuaji wa dhamira ya watendaji wa serikali katika kutoa taarifa za maendeleo kwa wananchi. Hasa zinazohusu mapato na matumizi yanayotokana na miradi ya maji kwenye maeneo yao," alisema Nguli.

Mradi huo ambao hadi kumaliza muda wake utatumia shilingi 40.00 milioni umetambulishwa kwa viongozi na watendaji 39 wa ngazi ya wilaya ya Lindi. Ambao waliongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Shaibu Ndemanga.