Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imejizatiti na ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba inaondoa fikra potofu kuhusiana na masuala ya kijinsia.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo jijni Dar e Salaam alipomuwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike (Girl Guides) katika masuala ya Uongozi ijulikanayo kama Julitte Low Seminar.
Amesema lengo la semina ni kupanua na kuimarisha ushiriki wa wasichana katika masuala ya girl guides lakini pia kuwawezesha kushirikiana katika masula ya kiutamaduni na uongozi ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo wasichana hao ili wazidi kufanya vizuri zaidi katika Jamii wanazotoka.
“Naamini baada ya semina hii ya siku saba wasichana watakuwa na uwezo kushiriki katika masuala ya uongozi na kukemea imani potofu ambazo zinakuwa zikionesha kuwa mwanamke ni kiumbe dhaifu na kutengeneza mtazamo chanya kuwa wanawake ni viumbe kama wanaume na wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu,”Alisema Prof Ndalichako.
Prof Ndalichako amesema Nchi ya Tanzania inatekeleza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia na kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanawake na wanaume wana fursa sawa katika maendeleo.
“Mhe Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu asingeweza kupata nafasi aliyo nayo kama nchi ingekuwa bado ina dhana potofu , uwepo wake ktk nafasi ya Makamu wa Rais, viongozi na wataamu wengine katika nyanja mbalimbali inaonesha kuwa nchi yetu imepiga hatua katika kuweka usawa wa kijinsia, ”aliongeza Prof ndalichako


