Tutatimiza dhamira ya Rais Magufuli - Naibu Waziri wa Nishati


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa dhamira ya Rais John Pombe Magufuli kuhakikisha vijiji vyote 12,319 nchini vinakuwa na umeme ifikapo Juni 2021 inawezekana na itatekelezwa kikamilifu na Wizara yake.

Ameyasema hayo leo, Novemba 10, 2019 katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu utekelezaji wa Ilani yake wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Amesema, kazi ya kuunganisha umeme vijijini inaendelea vizuri na kwamba kwa upande wa Wilaya ya Mkuranga, vijiji vipya 36 vineunganishiwa nishati hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.

 "Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, kulikuwa na vijiji 20 tu vyenye umeme Mkuranga. Sasa tumeongeza vingine 36 na kazi inaendelea." amesema.

Aidha, ameeleza kuwa, kupitia ziara zake za kuwasha umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkuranga akiwa amefuatana na Mbunge wa Jimbo hilo, Abdalah Ulega; wananchi takribani 1,200 wameunganishwa.

Naibu Waziri amempongeza Mbunge huyo wa Mkuranga kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia wizarani na TANESCO kuhusu utekelezaji wa miradi ya nishati jimboni kwake na kusema kuwa ni kiongozi wa mfano.

Akizungumzia sekta ya gesi, Naibu Waziri Mgalu amebainisha kuwa, viwanda takribani 50 vinatarajiwa kuunganishiwa gesi katika kipindi cha mwaka huu wa 2019.

Kwa upande wake, Mbunge Ulega ametoa shukrani nyingi kwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kwa kazi kubwa inayofanya, kuhakikisha watanzania wote wanafikiwa na umeme pasipo kubagua.
Naibu Waziri ameshiriki Mkutano huo akiwa ni mmoja wa waalikwa ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Katibu wa NEC (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa) Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga.