Urusi yaishtumu Marekani kuhusu udhibiti wa matumizi ya silaha

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergey Lavrov amesema kuwa ulimwengu unaendelea kuwa dhaifu kwa sababu Marekani haitaki kuzingatia utawala wa kudhibiti silaha.

Akizungumza wakati wa kongamano hukusu usalimishaji wa silaha mjini Moscow hii leo, Lavrov ameishtumu Marekani kwa kuchukulia mikataba ya kuthibiti matumizi ya silaha kuwa vikwazo katika juhudi zake za kuimarisha jeshi lake.

Mwaka huu, Urusi na Marekani zote zilijiondoa katika mkataba wa mwaka 1987 wa kudhibiti silaha za nyuklia za masafa ya kati.

Marekani inasema ilijiondoa kwa sababu ya ukiukaji wa Urusi, madai yaliyokanushwa na bunge la nchi hiyo.

Lavrov alithibitisha tena ahadi ya Urusi kutotumia makombora yaliyopigwa marufuku na mkataba huo hadi Marekani itakapofanya hivyo na pia kuwashutumu washirika wa Jumuia ya Kujihami ya NATO kwa kukataa kutoa ahadi sawa na hiyo.