Walichokizungumza Chama cha ADC kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa


Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimesema licha ya baadhi ya wagombea wake kuenguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kitashiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Katibu mkuu wa chama cha ADC, Hassan Doyo amezungumza na waandishi wa habari leo kwenye makao makuu ya chama hicho na kuweka wazi kuwa hawatajitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019.

Wakati ADC wakieleza hayo vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, UPDP, NLD, Chauma, ACT-Wazalendo na CUF vimeshatangaza kutoshiriki uchaguzi huo kwa madai ya kutotendewa haki ikiwa ni pamoja na wagombea wake wengi kuenguliwa.

“Sisi ni mabingwa wa changamoto hatupelekwi na mihemko ya watu, tunapelekwa na misingi ya chama cha siasa kwa sababu hata walipofuta matokeo ya uchaguzi Zanzibar wengine walisusa lakini sisi hatukufanya hivyo,” amesema Doyo

Doyo alitumia mkutano huo kumjibu katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliyedai kuwa wagombea wa upinzani walioenguliwa katika uchaguzi huo hawajui kusoma na kuandika.