Wataka ushirikiano katika Mipango Miji


Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe amesema  tofauti kubwa kati ya mipango ya kiuchumi na ile ya maendeleo ya ardhi ndiyo chanzo kikubwa cha kutokuwepo miji iliyopangika na kutaka kuwepo ushirikishwaji ili kuwa na miji iliyopangika.

Profesa Kombe alisema hayo hapo jana katika mahojiano maalum wakati wa kikao cha siku tatu cha Wataalamu wa Mipango kinachoendelea jijini Dodoma.

Alisema, kwa sasa mipango, sera na utekelezaji kuhusiana na masuala ya mipango miji vipo lakini tatizo kubwa ni tofauti katika mipango ya kiuchumi na maendeleo kwenye sekta ya ardhi kwa ujumla.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji ambayo iko chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, tatizo lingine linalochangia suala hilo ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusiana na manufaa wanayoweza kuyapata katika ardhi iliyopangwa.

 ‘’Mtu ukipanga ardhi yako unaongeza thamani hata kabla haijaongezewa huduma nyingine kama vile maji na umeme ndyo maana kuna tofauti kubwa kati ya anayeuza ardhi iliyopangwa na yule ambaye haijapangwa’’ alisema Profesa Kombe.

Alihimiza uwepo wa ushirikiano baina ya Serikali na sekta nyingine katika masuala mbalimbali yanayohusu upangaji miji ili kuepuka kuwa na maeneo yasiyopangwa ambayo mwisho wa siku ni kuwa na makazi holela.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa alisema, Mkutano wa wataalamu wa mipango miji unaoendelea unawakutanisha wataalaumu wote wa mipango miji kutoka serikalini na sekta binafsi ukiwa na lengo la kuboresha mipango miji nchini na kubainisha kuwa msisitizo mkubwa ni ushirikishwaji kwenye mipango ya matumizi ya ardhi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa City Plan Consultants (T) Limited Dkt Juma Mohamed aliiomba serikali kuipa kipaumbele mipango ya maendeleo ya ardhi kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu hususan katika masuala yanayohusu shughuli za binadamu.

Dkt Mohameda alisema, tatizo kubwa kwa wananchi wengi ni kutegemea matokeo ya haraka kwenye sekta hiyo wakati suala hilo linaweza kuhitaji mipango ya muda mrefu hasa katika masuala ya Mipango Kabambe.