Na Omary Mngindo-Bagamoyo
Wakazi wa Kitongoji cha Mtambani Kimarang'ombe Kata ya Nianjema Bagamoyo mkoani Pwani, wamemuomva Waziri William Lukuvi awasaidie waondokane na manyanyaso ya ardhi.
Wakizungumza na Waandishi wa habari katika eneo wanaloishi, Fatuma Ramadhani, Hussein Temo, Isdory Mwepong'we na Makolega Turuka, kwaniaba ya wenzao walielezea masikitiko yao ya kutakiwa kuondoka katika eneo waliloishi miaka 40 sasa.
Fatuma alisema kuqa walifika kwenye eneo hilo mwaka 1974 wakianza kulima, kabla ya Mkuu wa wilaya miaka hiyo Shaaban Kandolo kufika katika eneo hilo, akimtaka mmiliki kutokana na kuwa na pori kubwa.
"Alipofika alituuliza mmiliki, huku akitoa miezi mitatu kwa viongozi wamtafute mmiliki, na kutoa miezi mitatu, kama hajajitokeza eneo hilo ataligawa kwa wananchi waliokuwepo, huku akiwatqka viongozi wa Kijiji wakati huo na Kata kumfatuta," alisema Fatuma.
Nae Hussein Temo alisema kuwa baada ya muda aliouweka Mkuu huyo wa wilaya wakati huo kumalizika pasipokupatikana mmiliki, akaamua kuwagawia eka mojamoja kula mtu akaanza kuyaendeleza kwa kilimo, huku wengine wakijenga nyumba za muda.
"Tulishangazwa ulipofika mwaka 2010 kuwaona watu wakiwa na darubini wanapima maeneo hayo pasipokujulishwa, tuliitana na kukubaliana kwenda kwa viongozi wa Kijiji, ambapo Mwenyekiti akatuambia hata yeye hana taarifa ya zoezi hilo," alisema Temo.
Kwa upande wake Makolega Turuka alihoji uhalali wa Sud ambaye kwa sasa ni marehemu, ambaye ni mkazi wa Bagamoyo alikuwa wapi kwa zaidi ya miaka 40, na kuongeza kwamba hapo kun mchezo mchafu wa kutaka kuwaondoa wananchi hao kisha wapige bei.
"Tulimtafuta ofisa mtathimini akafanyakazi yake, akamtaka Sud atulipe fidia kutokana na sisi kukaa hapa kwa kipindi kirefu, lakini mpaka sasa tunasikia amefariki sisi hatujapata taarifa zozote, hata fidia yetu hatujui tutaipataje," alisema Makolega.
Akizungumzia sakata hilo, Afisa ardhi wilayani hapa Wendeline Izana alisema kuwa, taarifa hizo alipatiwa na Ofisa Mtendaji Kata ya kwamba eneo hilo ni la Omari Sud, aliwapatia wananchi hao walime mazao ya muda mfupi.
Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Yussuph Mgagala alisema kwamba analitambua eneo hilo miaka mingi kabla hajashika wadhifa huo, na kwamba linamilikiwa na Sud kabla ya kuwapatia wananchi hao walime mazao ya mida mfupi, na kwamba 2010 alifika kwa ajili ha kupima viwanja.
Mtendaji Kata wa Nianjema Sezary Madasha aliwaambia waandishi kwamba anatambua kwamba neo hilo ni la Sud, hivyo amewashauri wananchi hao wakafungue mashitaka katika mahakama ambayo ndio yenye maamuzi kisheria, wao viongozi wa serikali hawana uwezo wowote.

