Ridhiwani Kikwete awataka wakazi jimboni kwake kuchangamkia fursa hii


Na Omary Mngindo-Chalinze

Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Ridhiwani Kikwete, amewataka wakazi jimboni hapa kuchangamkia fursa ya Urasimishaji ardhi ili iweze kuwakomboa kiuchumi.

Aidha Mbunge huyo ameipongeza ofisi ya Mkurugnenzi wa halmashauri na watumishi wote kwa kushirikiana na  kampuni ya Amboni, kuweza kufanikisha zoezi hilo, huku akiitaka kampuni hiyo iongeze kasi ya kuwafikia wananchi wengine.

Ridhiwani ametoa rai hiyo kwenye hafla ya kukabidhiwa hati miliki wakazi 48 kati ya 100 waliomalizia taratibu zote, ikiwa ni baadhi ya wananchi 2000 waliopimiwa viwanja vyao kupitia mradi unaosimamiwa na wana-Chalinze wenyewe, kufuatia Kamati iliyoundwa chini ya Mwenyekiti wake Shamba Msakamali.

"Wakati zoezi likiendelea niliwahi kumwita Diwani Lucas Lufunga nikamuulizia uhakika wa kufanikisha zoezi hili, maana likiwa zuri la wachache likiharibika hata asiyehusika atajumuishwa," alisema Mbunge huyo.

 Aliongeza kwamba jambo lililofanyika ni la maendeleo kwa halmashauri akiwemo yeye mbunge na viongozi mbalimbali, huku akitaka kuongezwa kasi kwa zoezi hilo na kuwa mkakati ni kuhakikisha maeneo mengine ambayo hayajapimwa yapelekewe huduma hiyo.

"Hii hati inayotolewa leo na kwa wengine waliosalia haina tofauti na zinazotolewa Dar es Salaam maeneo ya Masaki, Mbezi na kwengineko, niwaombe wana-Chalinze tuchangamkie fursa hii muhimu ya kupimwa kwa maeneo yetu kwani itatupatia fursa ya kupata hati," alisema Ridhiwani.

Kwa upande wake afisa ardhi Mteule Zephania Sabo aliwataka wananchi kuchangamkia zoezi hilo, huku akiishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuwapatia fursa wananchi ya kupima viwanja vyao.

"Tuchangamkie zoezi hili, kwa mtu mmoja mmoja huwezi kulifanikisha kwani gharama inakuwa ya juu, niwaombe wananchi changamkieni fursa hii ya kupima maeneo yenu," alisema Sabo.

Diwani wa Kata Lufunga alielezea changamoto waliyokutana nazo wakati wakiendesha zoezi hilo, ambapo kulikuwa na vikwazo kutoka kwa wananchi waliopitiwa na mradi huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Shamba Msakamali amewataka wananchi ambao bado hawajalipia viwanja vyao tayari kwa kupatiwa hati hizo, wakalipie ili wakabidhiwe hati zao.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items