Naibu Waziri Mabula azitaka Halmashauri nchini kudhibiti ujenzi Holela



Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka halamashauri nchini kuhakikisha zinadhibiti ujenzi holela kwa kuhakikisha utoaji vibali vya ujenzi ktika maeneo yao unazingatiwa na kusimamiwa ipasavyo.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana katika halmashauri za wilaya za Morogoro, Mvomero pamoja na Manispaa ya Morogoro wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Morogoro.

Alisema, halmashauri nchini zina wajibu wa kudhibiti ujenzi holela katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na Watendaji wa Mitaa na kuweka taratibu ambazo hazitamruhusu mtu kufanya ujenzi wowote bila kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri husika. ‘’ ili kuondokana na ujenzi holela katika halmashauri zenu mwananchi asifanye ujenzi wowote bila kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri ‘’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zoezi la urasimishaji linaloendelea sasa katika maeneo mbalimbali siyo zoezi la kudumu na kulegalega kudhibiti ujenzi holela kutasababisha zoezi hilo kutokuwa na maana kwa kuwa ujenzi holela utakuwa ukiendelea.

Akigeukia suala la utoaji hati za ardhi, Dkt Mabula aliagiza Hati zilizokamilika katika ofisi za Msajili wa Hati wamiliki wake watangaziwe kupitia njia mbalimbali zikiwemo radio  za Kijamii (Local Radio) sambamba na hati hizo kutolewa kwa wamiliki wake katika eneo maalum litakaloandaliwa  karibu na maeneo wanaoishi wamiliki wa hati hizo.

Awali Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro Patrick Mwakilili alisema halmashauri yake imepanga kupima viwanja 1,000 kwenye  makao makuu ya wilaya Mvuha na viwanja 3,900 katika mji mdogo wa Kisaki ambao ni lango la kuingilia Mradi wa Kufufua Umeme wa Stiglers George na Hifadhi ya Mwl Nyerere zamani Selous.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya wilaya ya Morogoro,  tayari maeneo tisa ya kufanyiwa urasimishaji makazi yameanishwa ambayo ni Pangawe, Mkambarani, Fulwe, Ngerengere, Mvuha, Kisaki , Mtamba, Mkuyuni na Dhutumi na tayari halmashauri imepokea maombi ya kazi hiyo.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items