Waziri Simbachawene ataka lifanyike kongamano la mazingira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amesema ipo haja ya kufanya kongamano la taifa la mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambalo litawahusisha wadau ili kuboresha sekta hiyo.

Simbachawene amesema hayo wakati akipokea taarifa ya tathmini ya uharibifu wa uoto wa asili iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika maeneo ya Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni maagizo ya Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alipofanyika ziara mkoani humo mwanzoni mwa mwaka huu.


Waziri huyo alisema kuwa suala la mazingira linamhusu kila mtu hivyo kuna umuhimu wa kuwahusisha wadau kama wafanyabishara, sekta binafsi na taasisi za dini ambao watatoa mchango wa hali na mali katika kuchangia mfuko wa mazingira.

 “Upo umuhimu kwa Ofisi ya Makamu wa Rais na NBS kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kupata takwimu sahihi za hali halisi ya mazingira ili kuweza kukabiliana nazo na ningependa kuona pia utafiti na takwimu zichukuliwe katika mikoa mingine ikiwemo Geita, Singida, Dodoma na Tabora ambayo inaathiriwa na ukataji miti,” alisema.

Aidha alisisitiza kuwa masuala ya mazingira yaelekezwe katika ngazi ya Serikali za Mitaa ambako kule ni rahisi kuwafikia wananchikwa kutoa elimu kuhusu umuhimu wa  uhifadhi wa mazingira.