Ifahamu historia ya mchezaji Anthony Martial


Desemba 5, 1995 alizaliwa mchezaji wa soka wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Manchester United Anthony Martial. Alizaliwa mjini Massy, Essone nchini Ufaransa. Aliishi maisha yake ya ujana akiwa jijini Paris kuanzia mwaka 2001.

Martial alianza soka lake katika Les Ulis ya hapo hapo jijini Paris ikiwa ni klabu ambayo iliwalea na nyota wengine wakubwa wa soka ulimwenguni Thierry Henry na Patrice Evra.

Akiwa na umri wa miaka 12 aliruhusiwa kucheza soka akiwa na jozi moja ya kiatu cha mpira. Pia akiwa na umri huo alishawahi kufanya majaribu katika klabu ya Manchester City.

Alipofikisha umri wa miaka 14 ambayo ilikuwa mwaka 2009 alianza kuwinda na Olympique Lyon na walifanikiwa kumchukua ambapo alijiunga mwaka huo huo.

Akiwa katika msimu wa pili klabuni hapo aliingia katika rekodi ya kufunga mabao 32 katika mechi 21 za U17 na hiyo ikawa gia ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa chini ya umri wa miaka 17  kwa ajili ya mashindano ya Ulaya ya umri huo yaliyofanyika Slovenia.

Desemba 6, 2012 alianza kucheza soka la wakubwa akiwa na Lyon kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Europa dhidi ya Hapoel Ironi Kiryat Shmona ya Israel akitokea benchi na kumpokea Yassine Benzia kwenye dakika 10 za mwisho.

Katika mchezo huo huo Lyon walishinda mabao 2-0 kwenye dimba ya de Gerland. Mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu nchini Ufaransa (Ligue 1) alicheza Februari 3, 2013 dhidi ya Ajaccio ambako pia aliingia akitokea benchi katika dakika ya 79 akimpokea Rachid Ghezzal. Mchezo huo Lyon ilipoteza kwa kuzabuliwa mabao 3-1.

Baada ya hapo Martial alicheza tena mechi mbili akitokea benchi. Mnamo mwaka 2015 alitwaa tuzo ya Golden Boy ambayo hupewa mchezaji wa soka bora chini ya umri wa miaka 21 barani Ulaya.

Pia Martial ameshawahi kuitumikia AS Monaco ambapo alidakwa mnamo mwaka 2013 kwa ada ya euro milioni 6. Mnamo mwaka 2015 alisaini Manchester United kwa ada ya pauni milioni 36.

Alipotua tu Old Trafford alifunga mechi yake ya kwanza na mwezi huo huo alichukua tuzo ya mchezaji bora wa mwezi wa Ligi Kuu ya England.