Jinsi ya kumhudumia vyema mteja wako

Maisha na changamoto inakuletea njia za kutumia ili uwe na wateja wengi katika biashara yako,kazi yako,huduma yoyote unayotoa tumia njia hizo zitakusaidia.

 1. Kuwa na lugha nzuri kwa wateja.
Katika biashara yako ili uweze kuwapata wateja wengi, jijengee mazoea ya kuwa na lugha nzuri kwa wateja wako. Naelewa kuna wakati wateja wanakuwa wanakera sana. Lakini hilo lisikufanye ukamfokea mteji wako na kuanza kumrushia lugha isiyofaa. Mjali mteja wako na kumuonyesha lugha nzuri hata kama amekukera. Hiyo itakuwa ni njia bora ya kutoa huduma bora kwa wateja wako na itakupa sifa wewe na kupelekea kujenga biashara bora.

2. Ukaribisho mzuri kwa wateja.
Jenga mazoea ya kumkaribisha mteja wako vizuri. Mwonyeshe sura ya tabasamu ambayo hata bila kusema chochote itaashiria kwamba unamkaribisha kwa kumjali. Kuna watu ambao wanafanya biashara lakini utamaduni huu wa kumkaribisha mteja vizuri hawana. Kwa mfano kama una duka na mteja wako amefika na amekukuta unafanya kazi fulani. Achilia hiyo kazi na umsikilize mteja wako kwanza.

3. Kuwa na bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Siri kubwa ya kutoa huduma bora kwa mteja wako ni pamoja na kumpa mteja bidhaa zenye viwango vya juu. Kama utakuwa unatoa huduma bora inayoendana na thamani ya pesa ya mteja itasaidia sana kukuza wateja wako. Lakini hiyo haitoshi unapotoa huduma bora ya bidhaa inasaidia ili mteja akinunua bidhaa yoyote kwako anakuwa ana hamasa kubwa ya kurudi kwako tena kununua na hata kuwaambia wengine waje wanunue.

4. Jipe muda wa kuwasikiliza wateja wako.
Katika biashara kuna wakati huwa kuna malalamiko kutoka kwa wateja. Inawezekana kabisa mteja wako akawa hajaridhika na huduma fulani au ubora wa bidhaa unazotoa. Sasa inapotokea hali kama hii na akakwambia jifunze kuwasikiliza wateja wa namna hii na kufanyia mabadiliko mara moja. Ikiwa utamsikiliza na kufanyia kazi kile anachokitaka basi kesho elewa mteja huyo atakuwa wa kwako.

5. Mfanye mteja wako ajione wa thamani sana.
Unapokuwa kwenye biashara ni vyema ukajenga mazingira ya kumfanya mteja akijiona wa thamani. Mteja wako akishatambua hilo kwamba yeye ni wa thamani kwako, basi elewa kesho atakuwa ni wako tu hata iweje. Unaweza ukafanikiwa kwa hili ikiwa utajifunza kusimsikiliza mteja wako kwa makini, kujibu maswali yake vyema, ikiwezekana kwa mifano. Acha kupuuza chochote anachokwambia mteja wako, hata kama kinaonekana ni cha kijinga.

6.Kuomba msamaha kama bidhaa  ina mapungufu.
Inapotokea kwenye biashara yako kukawa kuna mapungufu fulani, omba msamaha haraka sana. Tuchulie wewe unafanya biashara ya kuuza chakula halafu ikatokea chakula hicho hakijawa kizuri sana. Ili mteja wako aridhike na huduma yako, njia bora hapo kwako ni kuomba msamaha mara moja. Kama utaomba msamaha na kuahidi kesho utampatia huduma bora zaidi basi atakuelewa na hata kuwa na hasira na wewe tena na atakuwa mteja wako kwa siku nyingine. Kwa kumueleza, hiyo itampelekea kujenga imani kubwa na wewe.

7. Kuokoa muda wa mteja.(acha kuwa busy ukiwa na mteja wako)
Pia huduma bora ni lazima iendane na kuokoa muda wa mteja. Acha kumfanya mteja wako kama mtoto kwa kumgandisha na kumpozea muda wake bila sababu. Mpe huduma mteja wako inayostahili kwa muda mwafaka. Kama unaona kuna eneo utachelewa ni bora ukamwambia ajue kuna kusubiri. Tatizo walilonalo wafanyabiashara wengi ni kuwapotezea wateja wao muda wakati mwingine bila sababu. Ili kuepuka kutokupoteza wateja, okoa muda wa mteja wako kwa kadri unavyoweza.

8 . Toa shukrani kwa mteja wako.
Mteja akishanunua kitu kwako au ukishampatia huduma ambayo wewe unatoa, jifunze kuwa na shukrani kwake. Mwambie tunashukuru kwa kuwa mteja wetu na karibu sana siku nyingine. Pia kwa kuongezea katika hili unaweza ukampa hata na mkono wa kumuaga. Unaweza ukaona ni kitu kidogo katika hili, lakini kitamfanya ajisikie vizuri na kesho atakuwa tayari tena kuweza kuja kwako.

Katika biashara wakati mwingine hauhitaji mtaji mkubwa sana ili kuweza kufanikiwa. Ila kwa kujijengea tabia ya kuwa na huduma bora kwa mteja ni njia nzuri sana ya kukuhakikishia mafanikio makubwa kibiashara. Chukua hatua na kuamua kutoa huduma bora kwa mteja wako