Mamilioni ya watu bado wanaambukizwa malaria - WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mamilioni ya watu bado wanaambukizwa malaria kila mwaka na zaidi ya 400,000 wanakufa kutokana na ugonjwa huo.

WHO imesema wengi wa wanaokufa ni watoto kutoka kwenye bara la Afrika. Shirika hilo limeonya kuwa ufadhili kwa ajili ya kupambana na malaria duniani ambao unasababisha kifo cha mtoto mmoja kila dakika mbili, bado unasuasua.

Ripoti hiyo imezitaka nchi wahisani na serikali za nchi zilizoathirika na malaria kuongeza juhudi za kupambana na ugonjwa huo.

Visa vya mwaka 2018 vilipungua kidogo hadi milioni 228 kutoka milioni 231 mwaka 2017 na vifo vilikuwa 405,000 kutoka 416,000 mwaka 2017.

Ripoti ya WHO imegundua kuwa wajawazito na watoto barani Afrika wanaendelea kuteseka na janga la malaria.