Rais Trump kuungana na viongozi wenzake wa NATO

Rais wa Marekani, Donald Trump na viongozi wenzake wa Jumuia ya Kujihami ya NATO wanakutana leo wakati ambapo mivutano baina ya baadhi ya nchi kubwa wanachama inatishia kudhoofisha uaminifu wa muungano huo wa kijeshi.

Viongozi wa nchi 29 wa NATO wanakutana kwa nusu siku kwenye hoteli ya kifahari nje ya mji wa London, Uingereza. Viongozi hao wanatarajiwa kuchapisha tamko linaloelezea nia yao katika kuadhimisha miaka 70 ya NATO na kuonyesha kuwa jumuia hiyo inakabiliana na vitisho vya sasa na wapinzani wapya kama China. Jana Trump na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron walizozana kuhusu ukosoaji wa Macron ambaye alisema NATO inahitaji kuzinduka na alilalamikia kukosekana kwa uongozi wa Marekani.

Marekani ndiyo mwanachama mwenye ushawishi mkubwa ndani ya NATO.