Wananchi watakiwa kuacha matendo ya ukatili wa Kijinsia



Na Paschal Malulu-Kahama.

Wananchi na wakazi wa halmashauri ya mji wa Kahama wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuachana na matendo ya ukatili kwa wanawake na watoto ili kuweka usawa katika jamii.

Akizungumza na Mwandishi wa Muungwana Blog, Afisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya mji wa Kahama Jonathan Shayo amesema ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ndani ya halmashauri hiyo ni mkubwa kutokana na kupokea mashtaka 350-600 kwa mwezi.

 Amesema katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili duniani wao kama dawati la kushughulikia masuala ya ukatili wanatoa elimu katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni ili kila mtu mmoja awe balozi wa kuhakikisha unyanyasaji wa kijinsia unaisha ndani ya halmashauri hiyo.

Shayo amesema katika mashtaka hayo kwa wanawake na watoto mengi ni ya kutelekeza hivyo wao kama ustawi wa jamii wanatoa elimu kila sehemu ambapo mafanikio yameanza kuonekana kwa baadhi ya wananchi kuanza kutoa taarifa za ukatili katika vyombo mbalimbali ili hatua zaidi kuchukuliwa.

“Tumekuwa tunatoa elimu katika ngazi za Kata na mitaa ambapo hadi imefikia wananchi watoa taarifa polisi, wengine wanakuja mpaka kwetu na tunachukua jukumu la kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake hivyo kwa sasa nafikiri baada ya muda ukatili utapungua hadi kuisha kabisa”amesema Shayo.

Amesema anaishauri jamii kuacha kuwanyanyasa watoto na wanawake kwani nao wanahitaji kupata haki zao za msingi katika nchi huku akiongeza kuwa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili zitamalizika Disemba 10 mwaka huu ambazo zilianza Novemba 25, 2019 na Kaulimbiu yake isemayo: “Kizazi chenye usawa simama dhidi ya ubakaji”.