Vijana waliogombea serikali za mitaa Kahama, CCM yawapongeza


Na Paschal Malulu-Kahama

Chama cha mapinduzi (CCM) wilayani Kahama mkoani Shinyanga kimesema kinawapongeza vijana wa chama hicho kwa kujitokeza kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2019 na kushinda katika nafasi za uongozi.

Kimesema katika mitaa 35 ya Wilaya ya Kahama, mitaa 24 inaongozwa na vijana ambao walijitokeza kugombea sawa na asilimia 68.57 huku vijiji 107 vimechukuliwa na vijana kati ya vijiji 246 kwa majimbo yote matatu ya Ushetu, Msalala na Kahama mji huku vitongoji  714 kati ya 1150 vinaongozwa na vijana.

Akizungumzia ushiriki wa vijana katika kugombea katibu hamasa na chipukizi wilayani Kahama Idd Chacha amesema miaka ya nyuma vijana walikuwa hawashiriki kwa kisingizio kuwa nafasi hizo ni za wazee lakini kutokana na hamasa ndani ya chama vijana wameelewa na kujitokeza kugombea.

Amesema katika majimbo yote matatu ya wilaya Kahama vijana walioshinda ni kati ya umri wa miaka 18-40 hivyo vijana wametambua umuhimu wa kuitumikia jamii katika maendeleo.

 Chacha amesema kazi za uongozi wa serikali za mitaa vijana walikuwa hawajitokezi kugombea kutokana na kukosa maslahi lakini kwa sasa wamejitokeza kuwatumikia wananchi licha ya kutokuwa na malipo na kuacha kukaa vijiweni bila kazi ya kufanya.

Aidha amesema kwa ushiriki huo vijana wamejitahidi kitendo hicho kinapaswa kupongezwa na wao kama wanahamasa wanawaasa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi kwa weledi bila ubaguzi ili kuchochea chachu ya maendeleo ya taifa kwani miaka ya nyuma ni asilimia ndogo kati ya 15-20 vijana walikuwa wakishiriki uchaguzi.