Waziri Jafo atangaza waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza, 2020


Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ametangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2020 kuwa ni 701,038 sawa na asilimia 92.27 ya wanafunzi 759,000 waliofaulu.

Akizungumza na waandishi wa jana Jijini Dodoma Mhe. Jafo ameeleza kuwa wavulana waliochaguliwa ni 335,513 sawa na asilimia 47.86 na wasichana 365,525 sawa na asilimia 52.14.

Mhe. Jafo alifafanua kuwa kwa mwaka 2019 jumla ya wanafunzi 759,737 walifaulu sawa na asilimia 81.3 ya waliofanya mtihani, wakiwemo wavulana 363,999 sawa na asilimia 47.9 na wasichana 395,738 sawa na asilimia 52.08.

Kati ya waliofaulu wamo wanafunzi wenye Ulemavu 1,461 sawa na asilimia 0.19 wakiwemo wavulana 777 na wasichana 684 aliongeza Jafo.

“ Kati ya wanafunzi waliochaguliwa, wanafunzi 3,145 sawa na asilimia 0.41 ya waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni, wanafunzi 970 watajiunga na shule za Wanafunzi wenye Ufaulu Mzuri zaidi; wanafunzi 1095 watajiunga na shule za Ufundi na wanafunzi 1,080 watajiunga na shule za bweni kawaida” alisema Jafo.

Aidha, wanafunzi 697,893 sawa na asilimia 99.59 wakiwemo wavulana 361,866 na wasichana 395,692 wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kutwa katika kata mbalimbali nchini aliongeza Jafo.

Waziri Jafo aliongeza kuwa Mikoa 13 ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora imeweza kuwachagua wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na Kidato cha kwanza mwaka 2019 katika shule za Sekondari za Serikali.

Aidha, jumla ya wanafunzi 58,699 sawa na asilimia 7.73 wakiwemo wavulana 28,567 sawa na asilimia 48.53 na wasichana 30,132 sawa na asilimia 51.33 ya waliofaulu, hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa alisema Jafo.

“Mikoa yenye uhaba wa vyumba vya madarasa na idadi ya wanafunzi waliobaki ni Arusha (4,739), Dar es salaam (5,808), Iringa (3,480), Kigoma (12,092), Lindi (1,695), Manyara (728), Mara (9,493), Mbeya (2,716), Pwani (2,918), Rukwa (686), Simiyu (6,616), Songwe (4,684) na Tanga (3,044)” alisema Jafo.