Waziri Kigwangalla aitaka TAWIRI kuweka mpango kazi wa kuwalinda Twiga


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamis Kigwangalla ameitaka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Nchini (TAWIRI) kuwa na mpango kazi wa mnyama aina ya Twiga katika hifadhi mbalimbali hapa nchini kwani kuna viashiria vya wanyama hao kutoweka katika hifadhi za Taifa.
 
Dkt Kigwangalla ameyasema hayo leo jijini Arusha,wakati akifungua kongamano la 12 lililoshirikisha nchi 16  wana sayansi watafiti wa uhifadhi duniani,Wakurugenzi na watendaji wa Taasisi za Uhifadhi nchini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali lililoandaliwa na Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania.

Amesema kuwa, katika mpango kazi wao wa miaka mitano wa utafiti wa wanyama TAWIRI wanapaswa kuweka mkazo wa kujuwa nini kinasababisha Twiga kutoweka katika hifadhi za Taifa na kuja na majibu ya msingi juu ya hali hiyo ili serikali iweze kutafanyia kazi haraka iwezekanavyo.

Waziri amesema Twiga ni nembo ya Taifa hivyo ni wajibu wa watafiti wa taasisi ya TAWIRI kuhakikisha wanapata majibu ya msingi kuhakikisha mnyama huyo hatoweki bali anaongezeka katika mbunga za Taifa.

Amesema kuwa, utafiti mwingine ambao TAWIRI inapaswa kuufanyia kazi ni pamoja na ndege wa Magharibi mwa Tanzania na kusema kuwa ndege hao ni kivutio kikubwa katika kuvutia watalii hapa nchini.

Dkt Kigwangalla amesema kuwa,katika ukanda huo kuna ndege aina  700 hupatikana katika eneo hilo la Magharibi mwa Tanzania hivyo ,Taasisi hiyo ya wanyama inapaswa kufanyia kazi na kuyapeleka mapendekezo yake serikali.

Waziri ameagiza TAWIRI kuweka nguvu zaidi kati suala la migogoro ya binadamu na wanyama kwani changamoto hiyo imekuwa kubwa  sana hapa nchini karibu hifadhi zote hapa nchini hivyo lazima taasisi hiyo ifanye utafiti wa kina wenye lengo la kupunguza ama kumaliza tatizo hilo.
Amesema utafiti huo unapaswa kuja na jibu la msingi lenye tija kwa pande zote mbili ili mnyama awe salama kwa faida ya uhufadhi na binadamu pia anapaswa kuwa salama na kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Aidha Waziri aliitaka TAWIRI walifanyie kazi  swala la  mito kwani wanyama aina ya Mamba na Kiboko wamekuwa wakiwala binadamu mara kwa mara pindi binadamu anapokwenda katika mito aidha kuchota maji ama kunywesha mifugo.

Amesema kuwa, tafiti zote zikipelekwa serikalini na kufanyiwa kazi ana uhakika migogoro kati ya binadamu na wanyama huenda ikaisha ama kupungua.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI,Dokta Saimon Mduma amesema kuwa, changamoto zote zilizosemwa na Waziri asilimia kubwa zimeshaanza kufanyiwa kazi na mapendekezo yake yatafikishwa serikalini kwa utekelezaji.

Dkt Mduma ametoa mfano wa eneo ambalo tayari wameanza kulifanyia kazi ni pamoja na eneo la mito kwa Mamba na kiboko kujengewa uzio ili binadamu wawe salama pindi wanapokwenda katika mito kuchota maji ama kunywesha mifugo yao.

Amesema kuwa, kuhusu mgogoro kati ya wanyama wakali kama tembo na simba kwenda katika maeneo ya raia na kuua binadamu na mifugo , TAWIRI imeshaanza kulifanyia kazi na watakuwa na majibu ya msingi nini kifanyike kwa serikali kumaliza mgogoro huo.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti wa TAWIRI, Dkt Julius Keyyu amesema kuwa, katika utafiti wa Twiga duniani imeonyesha kupungua kwa mnyama huyo katika hifadhi ,hivyo ni wajibu wao hapa nchini kuhakikisha nembo hiyo ya Taifa inaongezeka katika mbugani kutoka Twiga 29,000 kwa sensa ya mwaka 2016.

Dkt Keyyu amesema kuwa, sababu kubwa inayochangia kwa asilimia kubwa Twiga kupungua katika hifadhi ni pamoja na magonjwa mbali ya ngozi na masikio na wao wanajipanga kuhakikisha tiba inapatikana  ili suala hilo liweze kupotea kabisa.

Amesema kuwa,hivi  sasa TAWIRI imeweka mpango kazi wa miaka mitano wa kuhakikisha nembo hiyo ya Taifa inaongezeka katika hifadhi mbalimbali  hapa nchini ikiwa ni pamoja na kupambana  na magonjwa wanayokutana nayo na kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa Twiga na kumlinda mnyama huyo.