Bandari kavu ya Isaka kujengewa ofisi ya Zimamoto na uokoaji-Kahama


Na Paschal Malulu-Kahama



Jeshi la zimamoto na uokoaji wilayani Kahama mkoani Shinyanga linatarajiwa kufungua ofisi katika halmashauri za Ushetu na Msalala pamoja na kukarabati magari yake matatu ili kukabiliana na majanga ya moto katika halmashauri hizo.

Hayo yamesemwa na kamishna wa utawala na usimamizi wa fedha wa jeshi hilo Mbaraka Semwanza kuwa kutokana na wilaya ya Kahama kukua kwa kasi watafungua ofisi katika halmashauri za Msalala na Ushetu ili kusogeza huduma kwani kwa sasa huduma zote za zimamoto na uokoaji zinapatikana katika halmashauri ya mji wa Kahama pekee.

Amesema wadau mbalimbali wameanza kujitokeza wakiwemo TAMESA ili kusaidia utengenezwaji wa magari mabovu hivyo yakitengenezwa licha ya uchache wa watumishi yatasaidia kuwahudumia wananchi huku akisema jeshi hilo limewekeza nguvu kutoa elimu ya majanga ya moto kwa wananchi ili kukabiliana nayo.

Semwanza amesema licha ya kuanza mchakato wa kupata ofisi lakini pia wameiomba halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuwapatia eneo la kujenga ofisi katika bandari ya nchi kavu ya Isaka ili kusogeza huduma karibu zaidi kwani kwa kwa sasa bandari hiyo haina zimamoto.

Kwa upande wake kamanda wa Zimamoto na uokoaji wilayani Kahama Mohamed Dumah amesema wanaishukuru mamlaka ya utawala na usimamizi wa fedha kwa kuona changamoto inayowakabili katika kuwahudumia wananchi hivyo pindi magari yao yatapotengenezwa watayagawa katika halmashauri za Ushetu na Msalala.

Dumah amesema magari yao mabovu yakitengenezwa watakuwa na jumla ya magari matano ambayo yanafanya kazi hivyo watayagawa kwa halmashauri ya Ushetu na Msalala na halmashauri ya mji wa Kahama itabakiwa na gari moja lenye ujazo wa lita 16,000 huku akiwataka wananchi wanaoishi mabondeni wahame katika kipindi hiki cha masika.

Aidha kamishna wa utawala na usimamizi wa fedha Mbaraka Semwanza leo Januari 8, 2020 amefanya ziara ya kikazi ili kuona utendaji wa kazi wa jeshi hilo pamoja na kubaini changamoto ambapo amesema licha ya changamoto hizo jeshi hilo litaendelea kuwahudumia wananchi ipasavyo huku akiahidi changamoto zote zitaendelea kufanyiwa kazi.

Mpya zaidi Nzee zaidi