Kwa sasa Hiddink anaifundisha timu ya taifa ya China chini ya umri wa miaka 23. Alizaliwa Varsseveld na alianza medani ya soka akiwa kija katika klabu ya Varsseveld. Baadaye aliendelea katika klabu ya De Graafschap mwaka 1967.
Hiddink alicheza pia katika klabu ya Doetinchem chini ya kocha Piet de Visser. Mnamo mwaka 1973 Hiddink akiwa mikononi mwa kocha de Visser waliipandisha ligi kuu nchini Uholanzi Eredivisie. Akiwa kiungo katika soka la Uholanzi aliwahi kuzitumikia klabu nyingine kama PSV Eindhoven na NEC Nijmegen. Pia kuna nyakati aliwahi kwenda nchini Marekani. Alistaafu kucheza soka mwaka 1982 na kuanza hapo Hiddink amekuwa akifundisha soka katika klabu mbalimbali.
Mnamo mwaka 1987 Hiddink alitangazwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya PSV baada ya kuhudumu klabuni hapo kama kocha msaidizi. Akiwa na PSV kama kocha mkuu aliipa mataji matatu mfululizo ya Eredivisie pia mataji matatu mfululizo na taji la Ulaya Pia Hiddink aliweka rekodi muhimu msimu wa 1987-88 alipochukua mataji matatu tofauti. Pia Hiddink hakufanikiwa sana alipokuwa kocha mkuu wa Fenerbahce ya Uturuki. Baada ya kushindwa nchini Uturuki alipata nafasi nchini Hispania katika klabu ya Valencia alikokaa hadi Novemba 1993.
Alirudi tena Mestalla mnamo Machi 1994 alikokaa msimu mzima wa 1993-94. Hiddink alirudi nchini Uholanzi kuinoa timu ya taifa Januari 1995 ambapo aliiongoza kufika robo fainali ya UEFA Euro 1996 na pia kushika nafasi ya nne katika Kombe la Dunia mwaka 1998. Alijiuzulu baada ya kombe la dunia na baada ya hapo alitua Real Madrid ambako hakudumu sana kwani Februari 1999 alitimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa miamba hiyo katika La liga. Alisalia La liga katika klabu ya Real Betis mnamo February 2000 alikodumu kwa siku 90. Mnamo mwaka 2001 alipata nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya Korea Kusini na kuweka rekodi ya kuifikisha nafasi ya nne ya Kombe la Dunia mwaka 2002.
Alitua Chelsea baada ya kufahamiana na Roman Abramovich mwaka 2004 ambako de Visser aliyekuwa karibu na Abramovich alimtambulisha kwa Abramovich. Mnamo mwaka 2009 alitua Chelsea kama kocha wa mpito lakini alipata mafanikio makubwa alipokuwa Stamford Bridge akishinda Kombe la FA na kuirudisha Chelsea katika nafasi yake kwenye ligi. Aliondoka Chelsea na baadaye alirudi tena Desemba 2015 baada ya Jose Mourinho kutimuliwa.