Mkuu wa wilaya ya Temeke ajipanga kutokomeza biashara ya uchangudoa


Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bw.Felix Lyaniva amesema kwamba atahakikisha anatumia huduma ya  gari maalum la Mahakama Inayotembea mara kwa mara  ili kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe za saa za kazi,  uhalifu, uzururaji na uchafuzi wa mazingira katika eneo lake.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 24, mwaka huu  wakati Mahakama hiyo, ilipokuwa ikiendesha mashauri yaliyoletwa mahakamani  hapo  kwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi  Sokoine  Drive maarufu   kama ‘Mahakama   ya Jiji’ baada ya Manispaa ya Temeke, kufanya operesheni maalum na kuwakamata watuhumiwa hao wa makosa hayo.

Huduma hiyo iliyokuwa ikitolewa katika viwanja vya Zakhem vilivyoko Mbagala jijini Dar es Salaam.

‘Mahakama Inayotembea ni suluhisho la kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe saa za kazi na uhalifu.  Tunataka watu wafanye kazi halali na kufuata sheria za nchi,’ alisema Lyaniva huku akiongeza kwamba hataki kuona vitendo hivyo kwenye eneo lake.

Alisema watuhumiwa hao, walikamatwa na ushahidi ukiwepo.

Lyaniva aliongeza kwamba anaiomba Mahakama ya Tanzania, kutoa huduma  hiyo mara kwa mara kwenye wilaya hiyo, ikiwezekana kwa kila Ijumaa.

Akizungumza kuhusu watuhumiwa waliofikishwa mahakamani hapo, Mratibu wa Mahakama hiyo, Mhe Moses Ndelwa, ambaye pia ni Hakimu Mkazi alisema wako takribani 50.

Hivyo mashauri hayo yanasikilizwa, baada ya kupokea maelezo kutoka kwa waendesha mashitaka na wapelelezi.

Ndelwa  alifafanua kwamba watuhumiwa hao  wametonzwa faini ya Sh. 20,000  hadi 50,000 kulingana na makosa waliyotenda.

 Naye  Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Suzan Kihawa alisema watuhumiwa hao , wanakiri makosa ndio maana  makosa yao  hayahitaji uchunguzi  hali sababisha kusikilizwa kwa haraka.

Mashauri hayo yalisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive.

Wakati huohuo,  baadhi ya wakazi wa Mbagala, wakizungumza kwa nyakati tofauti, ambao ni Adamu Juma  alisema  tukio hilo limemfundisha  kwamba unaweza kukamatwa na kuhukumiwa hapo kwa hapo.

Wengine ni Hamisi Ally  umri wa miaka (22), Said Hemed (20), Eva Michael(40) na Abuu Ramdhani walisema wanaishukuru Serikali kwa kuleta huduma hiyo, ambayo inakwenda vizuri na kuwezesha mashauri kusikilizwa kwa wakati na kupunguza mlundikano wa mahabusu au kesi kuchukua muda mrefu.

Pia Mahakama hiyo itawasaidia kupunguza vitendo hivyo katika eneo hilo.