Serikali imeruhusu upimaji binafsi,ili kuendelea kupunguza maambukizi ya VVU-Faustine Ndungulile

Na Amiri kilagalila-Njombe

licha ya ripoti za maambukizi ya ukimwi kutajwa kupungua mkoani Njombe lakini kundi la vijana limeelezwa kuendelea kukumbwa na maambukizi mapya nchini kwa asilimia 40 na  wasichana ndio wahanga wakubwa zaidi katika kundi hilo.

Ripoti ya afya mkoa wa Njombe mbele ya naibu waziri wa afya iliyosomwa na dokta Manyanza Mponeja kwa niaba ya mganga mkuu wa mkoa imeeleza kuwa serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na maambukizi mapya ya ukimwi ikiwemo kuhamasisha jamii kujitokeza kupima vvu.

“Hadi sasa tumeweza kufikia 81% katika eneo la kufanya watambue,wanaotumia huduma tumefanikiwa kufubaza virusi vya ukimwi ndani yao kwa 90% hivyo tunaendelea na upimaji na juhudi mbali mbali ili kuhakikisha hao wengine tunwafikia pia”alisema Manyanza Mponeja

Naibu waziri wa afya dokta Faustine Ndugulile katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe anasema serikali kupitia bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania limepitisha sheria ya kuwataka vijana kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi pasina kusubiri ridhaa ya wazazi hatua ambayo itasaidia sana kuwatambua waathirika huku wito ukitolewa kwa wanaume kuacha woga wa kwenda kupima vvu.

“Maambukizi yameanza kuhamia kwa vijana wa miaka 15 mpaka 24 na asilimia kama 40 yapo kwa vijana,sasa hivi tumeshusha umri wa kupima mpaka miaka umri wa miaka 15 kwa hiyo kijana wa miaka 15 anaweza kupima virusi vya ukimwi bila ridhaa ya mzazi,lakini vile vile tumeruhusu upimaji binafsi,na tutaweka mfumo ambao mtu yeyote anweza kwenda kwenye maduka ya kununua dawa kulingana na utaratibu ambao tutauweka anaweza akanunua vitendanishi akajipima”alisema Faustine Ndugulile

Katika suala la kasi ndogo ya usambazaji dawa za afua za lishe naibu waziri ameutaka mkoa wa njombe kuchukua hatua za makusudi katika kutekeleza zoezi hilo.

Christopher Ole Sendeka ni mkuu wa mkoa wa Njombe ambaye anasema katika kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa ukimwi wamelazimika kuanzisha kampeni ya tohara katika kundi la watoto na wanafunzi baada ya kuwafikia zaidi ya wanaume laki moja.

“Tumefanikiwa kupitia asasi za kiraia katika kampeni hii ya tohara kinga,tumeshafikia wanaume watu wazima laki moja na tisini na sita,baadaye tumeamua kujielekeza zaidi hatua ya watoto wadogo,wa sekondari na shule za msingi”alisema Ole Sendeka