Amewataka kusimamia vizuri maendeleo ya elimu kwa kuhakikisha kila mwanafunzi ambaye amechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza anaripoti shuleni, kusoma mapato na matumizi kwa wananchi wao pamoja na kuhamasisha kilimo cha biashara hasa zao la Korosho.
DC Ndejembi amesema nia njema ya Rais Magufuli ya kutoa elimu bila malipo kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne inapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote kwani Taifa haliwezi kufikia Uchumi wa kati kama halitotilia mkazo maendeleo ya elimu nchini.
" Nyie wenyeviti na watendaji ndio mnaokaa muda mrefu na wananachi wetu, niwasihi msiruhusu wazazi wakakwamisha mtoto kujiunga na kidato cha kwanza. Tunahitaji kuona Wilaya ya Kongwa ikitoa wasomi wengi ambao watakua na msaada mkubwa kwetu na Taifa kwa ujumla.
Rais ametekeleza elimu bila malipo kwa kiwango kikubwa sana, mabilioni ya fedha yanatumika kila mwaka kwenye sekta ya elimu, tusikubali kuona mwanafunzi anakaa nyumbani kwa sababu mzazi kamwambia akachunge mbuzi au kakataa kumnunulia sare za shule, tuchukue hatua na muwaripoti wazazi wenye tabia hizo," Amesema DC Ndejembi.
Aidha amewataka wenyeviti wa vijiji kuzingatia utaratibu wa kuwasomea mapato na matumizi wananchi wao ili waweze kujua kiasi walichoingiza kwenye vijiji vyao na namna ambavyo uendeshaji wa miradi yao unaenda ili kuondoa migogoro inayoweza kuepukika.
Pia amewataka kutotumia nafasi walizopata kwa maslahi yao badala yake wajikite katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wao na siyo kusubiri mpaka kiongozi wa ngazi ya juu afike ili wananchi waeleze shida zao.
" Nyinyi ni watumishi wa wananchi, wao ndio waliowachagua nendeni mkawatumikie bila upendeleo. Watendaji wa kata nisisikie malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba mnawaomba kitu kidogo ili muweze kuwagongea mihuri. Sitomvumilia yoyote ambaye atashindwa kuwahudumia wananchi hawa wanyonge," Amesema.
Ametoa rai kwa viongozi hao kuhamasisha wananchi wao kufanya kilimo cha biashara kwa kuepukana na kilimo cha mazoea kwa kujikita haswa katika kilimo cha korosho ambacho wataalamu wa kilimo wamesema kinafaa ndani ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai amewataka viongozi hao kutumia dhamana waliyopewa katika kuwatumikia wananchi wanyonge na kamwe wasijaribu kuomba rushwa.
Amewasisitiza kuongeza mkazo kwenye elimu hasa kwa Kata za Mtanana na Mamlaka ya Kibaigwa ambapo wamekua nyuma katika ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne.
" Ndugu zangu hakuna mafanikio yoyote bila elimu, tujikite katika kutilia mkazo elimu tuwe wakali kwa wazazi ambao watashindwa kuwapeleka watoto wao shule ilihali hakuna malipo yoyote.
Toeni ripoti kwa DC tusiruhusu watoto wetu wakose elimu kwa sababu za ndani, nafahamu zipo changamoto za nje ambazo kwa hakika serikali inapambana kuzitatua lakini tumalize kwanza changamoto zetu za ndani tuone kama atutoongeza namba ya wanafunzi wanaofaulu," Amesema Mhe Ndugai.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa, Dk Omary Nkuru amesema kiwango cha ufaulu kwa matokeo ya kidato cha nne ndani ya Wilaya hiyo yameongezeka ambapo imekua ya pili kimkoa nyuma ya Jiji la Dodoma huku idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano ikiwa ni 670 kulinganisha na mwaka jana ambapo walikua 300.


