Vijana wametakiwa kujiunga kwenye vikundi, kunufaika na mkopo




Na James Timber, Mwanza.

Vijana nchini wameaswa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli zikiwemo mikopo inayotolewa na halmashauri zote nchini kupitia fedha za mapato yake ya ndani kwa kutenga 10%, 4% ikitolewa kwa vijana, 4% kwa wanawake na 2% kwa watu wenye ulemavu.

Rai hiyo imetolewa na mratibu wa mafunzo ya ujasiriamali na uwezeshaji kutoka taasisi ya Tanzania One Movement mkoa wa Mwanza Bi Lilian Emanuel Lambo wakati akiendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutoka kata ya Mirongo jijini Mwanza ambapo amesisitiza vijana kuwa waaminifu na kuthubutu kwa kuanzisha miradi itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi kutokana na uwepo wa fursa za mikopo, mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na wizara ya ofisi ya waziri mkuu, vijana, ajira na watu wenye ulemavu.


'.. Vijana wenzangu Serikali yetu imekuwa ikitoa fursa za kujikwamua kiuchumi ikiwemo utengwaji wa mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu, Tuzitumie fursa hizi na sasa mikopo haina hata riba ..' Alisema

Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii wa kata ya Mirongo Bi Wande Peter amefafanua sifa wanazotakiwa kuwa nazo vijana waliohudhuria mafunzo hayo ili waweze kukopesheka ikiwemo umri wa chini ya miaka 35, uwepo wa mradi unaoombewa fedha na kikundi kilichosajiriwa huku akiwataka kutoona usumbufu pindi wanapokosolewa ili kukidhi matakwa ya kukopesheka.


Akitoa ushuhuda moja ya vijana walionufaika na mafunzo ya ujasiriamali kutoka wizara ya ofisi ya waziri mkuu Sera, Bunge, Vijana na watu wenye ulemavu Ndugu Elisha Peter Magodola ameishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo sanjari na kuahidi kuwafundisha vijana wengine ili yaweze kuleta tija kwa jamii.

Mafunzo  ya Ujasiriamali yaliyotolewa yamefadhiliwa na Mbunge wa Viti maalumu  wa chama cha mapinduzi kupitia kundi la Vijana Mhe Bi Halima Bulembo kwa kushirikiana na taasisi ya Tanzania One Movement na kutarajiwa kuendelea kutolewa maeneo mbalimbali ya nchi ili kuwakwamua vijana kiuchumi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items