Watumishi wazembe Tanesco wakalia kuti kavu

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka,  amesema hatawavumilia watumishi wazembe ndani ya Shirika badala yake siku zao zinahesabika.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku sita kwa watumishi wapya 958 walioajiriwa hivi karibuni.

Watumishi hao wanaendelea na semina elekezi wakiwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma na wako katika vituo vitatu ambavyo ni Dodoma, Morogoro na Mtwara.

Dkt. Mwinuka amesema TANESCO ni shirika linalotegemewa katika ukuzaji wa  uchumi wa taifa hususani katika kipindi hiki ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda hivyo haiwezekani wengine wakawa wanakimbia halafu mwingine anatembea au amekaa.

Amewaambia watumishi hao wapya kuwa Serikali inawategemea zaidi kwa kuwa wameingia ili kuongeza kasi ya kufikia malengo ya kuzalisha megawati 10,000 ifikapo 2025.

"Serikali ina matumaini makubwa kutoka kwenu, mmeingia katika eneo linalotazamwa zaidi na wengi na kutegemewa hivyo lazima mtambue Serikali inategemea nini kutoka kwenu ili msiliangushe Shirika," amesema Dk. Mwinuka.

Wakati huo huo Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Dkt. Emanuel Shindika, amesema mafunzo kwa watumishi hao yanalenga kuboresha mifumo ya utendaji katika utumishi kwa wafanyakazi hao wapya.

Dk.Shindika amesema utumishi wa umma ni jambo jema kwa mtu anayeweza kuwatumikia watu lakini itakuwa aibu kwa anayeshindwa kufuata maadili na vigezo vya kiutumishi wakati wote.

Amewataka watumishi hao kuzingatia watakayofundishwa ili wanapofika kazini wasiwe na shida kwani semina elekezi huwa ni zaidi ya mafunzo ya vyuoni.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Astelia Sukulu amesema mafunzo hayo yatawasaidia kujua miiko na wajibu wao katika chombo cha umma huku akisisitiza watakuwa wenye kutunza siri za shirika.